![]() |
| Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) akizungumza na Menejimenti ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) leo Jijini Arusha. |
Na Mwandishi wetu
Arusha.
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limetakiwa kutumia
teknolojia ya kisasa kulinda na kuhifadhi maeneo yake kwa lengo la kuzuia
ujangili na uvamizi wa maeneo hayo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb)
ameyasema hayo leo Oktoba 28,2023 alipokuwa akizungumza na menejimenti ya
TANAPA katika Ofisi za Makao Makuu ya TANAPA jijini Arusha.
" Kuhusu kukabiliana na ujangili pamoja na kufanya doria
hifadhini tuendelee kuwa na matumizi ya vifaa vya teknolojia ya kisasa
kuhakikisha doria na ulinzi wa maeneo yetu unafanikiwa kwa asilimia
mia"amesema Mhe. Kairuki.
Amesema kwa kufanya hivyo, itawarahisishia utendaji kazi na
kuwezesha ulinzi wa maeneo ya hifadhi kwa njia ya kisasa zaidi.
Aidha, ameitaka TANAPA kuendelea kutangaza vivutio vya utalii
kidijitali ili kufikia idadi ya watalii milioni tano kama ilivyokusudiwa.
"Muendelee kujiimarisha katika matumizi bora na sahihi ya
kidijitali na pia mjikite katika kupata mrejesho wa huduma zinazotolewa kwa
watalii ili tuweze kuboresha huduma hizo" Mhe. Kairuki amesema.
Aidha, amewataka watumishi wa TANAPA kutekeleza majukumu yao kwa
kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo na kwa
kutumia busara ili kulifanya shirika hilo lisonge mbele.
Amefafanua kuwa ni vyema watumishi hao kutoa huduma bora za
haraka, zenye ufanisi na zenye matokeo makubwa ya kuvutia watalii.
Mhe. Kairuki pia ameitaka menejimenti ya shirika hilo kushughulikia migogoro kati ya hifadhi na wananchi kwa kuhakikisha inapatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo na kuendelea kuwa na mahusiano mazuri na wananchi kwa kuboresha ujirani mwema.
Naye, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Mussa Juma amesema
atahakikisha anafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na kuwa wabunifu
kuhakikisha shirika hilo linasonga mbele.
![]() |
| Baadhi ya Viongozi wa TANAPA. |



Post a Comment