![]() |
| MKUU wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda (Kushoto) akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa kituo cha kupozea Umeme wa njia kuu yenye msongo wa KV 220. |
![]() |
| Aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati, Medard Kalemani akiweka jiwe la Msingi ujenzi wa kituo cha kupozea umeme eneo la Imalilo Mkoani Simiyu Machi 03, 2021. |
Na Derick Milton, Simiyu.
Hatimaye matumaini mapya yameanza kuonekana kwa wananchi wa Mkoa
wa Simiyu, juu ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme (Sub station) baada ya
wakandarasi wa mradi huo kuanza kutekeleza kazi za awali.
Mradi huo unatekelezwa na wakandarasi wawili, ambapo mmoja
anatekeleza mradi wa ujenzi wa Njia kuu ya kusafirisha umeme ya msongo wa KV
220 Shinyanga hadi Simiyu na Mkandarasi wa pili anatekeleza ujenzi wa mradi wa
kituo cha kupozea umeme.
Machi 03, 2021 aliyekuwa Waziri wa Nishati wakati huo Medard
Kalemani, aliongoza hafla ya uwekaji jiwe la Msingi ujenzi wa kituo hicho eneo
la Imalilo Mjini Bariadi na kutoa matumaini kwa wananchi wa Mkoa huo,
kuondokana na adha ya kukatika mara kwa mara kwa umeme mara baada ya kukamila
kwa mradi huo.
Kalemani alihaidi kituo hicho kujengwa ndani ya Mwaka mmoja,
ambapo matumaini yalikuwa ujenzi huo ukamilike Machi 03, 2022, na ulitarajia
kugharimu zaidi ya Sh. Bilioni 75.
Hata hivyo mradi huo haukuwahi kutekelezwa tangu kuwekwa kwa
jiwe hilo msingi ikiwa imepita zaidi ya miaka mitatu huku matumaini ya wananchi
wa Mkoa huo kuondokana na adha ya umeme kukatika katika mara kwa mara yakianza
kupotea.
Matumaini hayo mapya yameanza kuonekana chini ya Rais Samia
Suruhu Hassan baada ya Juzi Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Yahya Nawanda kufanya ziara
katika Wilaya za Maswa na Bariadi ambako mradi huo unatekelezwa na kuzungumza
na wakandarasi.
Ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa imefufua matumaini hayo na kwamba
sasa mradi huo umeanza kutekelezwa, ambapo alitembelea kambi za wakandarasi hao
na kuzungumza nao.
Akitoa taraifa ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo, Meneja
mradi Mhandisi Adolf Kigombola alisema kuwa kazi za awali zimeanza kutekelezwa
na mkandarasi baada ya TANESCO kwa kushirikiana na wadau wa mradi kufanya
uhamasishaji kwa Wananchi ili kuruhusu uanzaji wa kazi za awali wakati Serikali
ikichakata malipo ya Fidia.
Alisema kuwa TANESCO inafuatilia kwa karibu malipo ya fidia kwa
waathirika wa mradi na kwamba Wananchi watarajie malipo ya fidia mapema Mwezi
Novemba 2023.
Mkuu wa Mkoa aliwataka wakandarasi hao kuhakikisha wanatekeleza
mradi huo, ndani ya muda uliopangwa, ili wanancha wa Mkoa wa Simiyu waweze
kuondokana na adha ya kukatika katika kwa umeme mara kwa mara.
"Tunataka ndani ya miezi 18 kipindi cha Mkataba mradi uwe
umekamilika na utekelezaji wa mradi usiwe na mashaka mashaka na
wamenihakilishia hapa kuwa kazi hii itakamilika ndani ya muda uliopangwa"
alisema Dkt. Nawanda
Mkandarasi M/S Kalpataru Projects International Limited (KPIL)
kutoka Nchini India anatekeleza ujenzi wa Njia kuu ya kusafirisha umeme ya
Msongo wa KV 220 na M/S Sian Electric Engineering Co.LTD akitekeleza ujenzi wa
kituo cha kupozea umeme.


إرسال تعليق