RC Simiyu atembelea na kukagua ujenzi wa kituo cha Kupoza Umeme.

MKUU wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda (Kulia) akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa kituo cha kupozea Umeme wa njia kuu yenye msongo wa KV 220.



Na Mwandishi wetu, Bariadi.

 

MKUU wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda ametembelea na kukagua ujenzi wa kituo cha kupozea Umeme na kuwaagiza wakandarasi wanaotekeleza mradi kukamilisha kwa wakati ili wananchi wapate umeme wa uhakika.

 

Mradi wa Njia kuu ya kusafirisha umeme ya Msongo wa KV 220 Shinyanga (Ibadakuli) hadi Simiyu (Bariadi), pamoja na ujenzi wa kituo cha kupooza umeme cha Simiyu unatarajiwa kujengwa na kwamba ukikamilika utaondoa adha ya kukatika kwa umeme mara kwa mara Mkoani Simiyu.

 

Dkt. Nawanda ametoa maagizo hayo jana (25 Oktoba 2023) katika ziara yake kwenye Wilaya ya Maswa na Bariadi iliyolenga kukagua utekelezaji wa mradi huo.

 

"Tunataka ndani ya miezi 18 kipindi cha Mkataba mradi uwe umekamilika na utekelezaji wa mradi usiwe na mashaka mashaka na wamenihakilishia hapa kuwa kazi hii itakamilika ndani ya muda uliopangwa" alisema Dkt. Nawanda.

 

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa, ameshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufikisha umeme katika vijiji 470 ndani ya Mkoa wa Simiyu.

 

"Katika Nchi hii, ni Mkoa wa Simiyu pekee ambao hatumdai Mhe. Rais Samia katika kijiji chochote na kazi yetu tuliyo nayo ni kusafirisha umeme katika Vitongoji baada ya umeme huu kuongezewa Nguvu baada ya kukamilika mradi huu unaotekelezwa wa kusafirisha umeme kV 220" alisema Dkt.Nawanda.

 

Kwa upande wake Meneja wa mradi huo Mhandisi Adolf Kigombola alisema tayari kazi za awali zimeanza kutekelezwa na mkandarasi baada ya TANESCO kwa kushirikiana na wadau wa mradi kufanya uhamasishaji kwa Wananchi ili kuruhusu uanzaji wa kazi za awali wakati Serikali ikichakata malipo ya Fidia.

 

Aidha aliongeza kuwa TANESCO inafuatilia kwa karibu malipo ya fidia kwa waathirika wa mradi na kwamba Wananchi watarajie malipo ya fidia mapema Mwezi Novemba 2023.

 

Mkandarasi M/S Kalpataru Projects International Limited (KPIL) kutoka Nchini India anatekeleza ujenzi wa Njia kuu ya kusafirisha umeme ya Msongo wa KV 220 Shinyanga (Ibadakuli) hadi Simiyu (Bariadi), huku kituo cha kupoozea umeme ujenzi wake ukitekelezwa na M/S Sian Electric Engineering Co.LTD.

 

MWISHO.

 

MKUU wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda (Kushoto) akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa kituo cha kupozea Umeme wa njia kuu yenye msongo wa KV 220.

 

Picha ya Pamoja.



Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda (katikati) akionyeshwa maandalizi ya ujenzi wa kituo cha kupozea umeme.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda (katikati) akitembezwa na kuonyeshwa maandalizi ya ujenzi wa kituo cha kupozea umeme.

 

MKUU wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda (Kulia) akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa kituo cha kupozea Umeme wa njia kuu yenye msongo wa KV 220.

 

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post