Madarasa
mawili na Ofisi ya Walimu iliyojengwa na TASAF katika shule ya Msingi Mwawayi
wilaya ya Maswa.
Na Samwel Mwanga, MASWA.
WAKUU wa Divisheni na Vitengo katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu wameridhika na miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia Miradi ya kupunguza umasikini TPRP IV-OPEC IV wilayani humo.
Wamesema hayo, Oktoba 3 mwaka huu, mara baada ya kutembelea miradi hiyo iliyoko katika Jimbo la Maswa Mashariki na mafanikio hayo yametokana na ushirikiano uliopo baina ya viongozi, wataalamu na wananchi.
Wamesema kuwa wameamua kufanya ziara hiyo maalum ya kukagua miradi ya Wananchi inayotekelezwa na TASAF kwa lengo la kuwajengea uelewa wa pamoja kwa Wakuu hao.
"Kufanya kazi kwa ushirikiano ndio kumepelekea miradi hii kukamilika kwa kiwango kikubwa na kwa ubora kama tulivyoiona wakati wa ziara yetu tulipoitembekea, "amesema Mussa Mwita ambaye ni Mwanasheria wa Halmashauri hiyo.
Walisema kuwa wamejifunza kushirikiana kwa ukaribu zaidi kati ya Serikali na wananchi ni jambo la muhimu ma ndiyo hali iliyosababishai kukamilishwa kwa miradi na kwa wakati.
"Mie hapa nimejifunza jambo moja kubwa sana kuwa mafanikio haya ya kutekelezwa kwa miradi ya Tasaf kwa wakati imetokana na ushirikiano wa karibu kati ya serikali na wananchi,"amesema Simeon Makuru ambaye ni Afisa Biashara wa halmashauri hiyo.
Aidha wamewashauri wataalamu kutoka TASAF katika halmashauri hiyo kuwa maeneo ya vijijini yanayofanya kazi vizuri katika kutekeleza miradi yaongezewe fedha za miradi mingi zaidi ili iwe kama motisha kwa wengine kufanya vizuri zaidi.
Pia wametoa wito kwa wananchi waendelee kutunza miradi hiyo ili ilete manufaa zaidi kwao na vizazi vijavyo.
Naye Mwezeshaji wa TASAF, Issack Singu ambaye ni Afisa Mazingira wa Tasaf amesema kuwa miradi mingi imeibuliwa na wananchi wenyewe kwenye maeneo yao kutokana na changamoto wanazokuwa wanakutana nazo.
"Hii miradi yote tuliyoitembelea imeibuliwa na wananchi wenyewe kulingana na changamoto zilizokuwepo katika maeneo yao ndiyo maana unaona ushiriki wao ni mzuri kwenye miradi hiyo,"amesema.
Mratibu wa TASAF wilaya ya Maswa, Grace Tungaraza amesema kuwa katika utekekezaji wa miradi hiyo ya Tasaf kwa mwaka wa fedha 2021/2022 halmashauri hiyo ilipokea kiasi Cha Sh 1,020,721,737.87 kwa ajili ya kutekeleza miradi 15 ikiwemo ya uboreshaji wa Miundombinu 10, kukuza uchumi kaya miradi miwili na Ajira za muda tatu.
Ameongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023,Mei 5 mwaka huu pia wamepokea Shilingi 451,927,281 kwa ajili ya miradi Mitano ya uboreshaji miundo mbinu ya Elimu na Afya.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na Ujenzi wa Bweni la Wasichana 80 katika shule ya Sekondari Budekwa kwa gharama ya Sh Milioni 89.5,Ujenzi wa madarasa mawili,Ofisi ya Walimu na Matundu sita ya choo katika shule ya Msingi Mwawayi kwa gharama ya Sh Milioni 76.7 na Ujenzi wa nyumba ya Mganga katika Zahanati ya Mwabayanda M kwa gharama ya Sh Milioni 55.5
Miradi mingine ni pamoja na Ujenzi wa madarasa mawili,Ofisi Moja ya Walimu na Matundu sita ya choo katika shule ya Msingi Mwafa kwa gharama ya Sh Milioni 70.1,Ujenzi wa zahanati Kijiji Cha Mwakidiga kwa gharama ya Sh Milioni 103.8 na Ujenzi wa zahanati katika Kijiji cha Bushitala kwa gharama ya Sh Milioni 103.8
Ziara ya kukagua miradi ya TASAF kwa halmashauri ya Wilaya ya Maswa imefanywa kwa lengo la kujengeana uelewa wa pamoja Wakuu wa Divisheni na Vitengo kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo kwa ngazi ya halmashauri.
MWISHO.
Mwalimu
Alponary Mwinyi wa shule ya Sekondari Budekwa wilayani Maswa(aliye
kati)akiwaelezea Wakuu wa Divisheni na Vitengo katika halmashauri ya Wilaya
hiyo faida za Bweni la Wasichana lililojengwa na TASAF.
Madarasa
mawili na Ofisi ya Walimu iliyojengwa na TASAF katika shule ya Msingi Mwawayi
wilaya ya Maswa.
Ujenzi
wa Bweni la Wasichana wapatao 80 katika shule ya Sekondari Budekwa wilaya ya
Maswa lililojengwa na TASAF.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com


إرسال تعليق