Kampeni hiyo imezinduliwa leo Mkoani Morogoro, ambapo
ilitanguliwa na mafunzo kwa waandishi wa habari zaidi ya 20 kutoka katika mikoa
mbalimbali tanzania bara na visiwani yaliyolenga kupiga vita vitendo vya
ukatili wa kijinsia.
Akizundua Kampeini hiyo kwa niaba ya Rais wa UTPC Deo
Nsokolo, Mjumbe wa Bodi ya UTPC Lilian
Lucas amesema kuwa waandishi wa Habari wanayo nafasi kubwa kupitia kalamu zao
kuhakikisha vitendo hya ukatili kwa wanawake na watoto vinakomeshwa.
“ Kwa sasa tuna tatizo kubwa la matukio ya ubakaji na
ulawiti wa watoto wa kike na wadogo, kupitia kampeni hii tunaomba wanahabari
kuungana kwa pamoja na wadau wengine kuweka nguvu zaidi za kuhakikisha
tunakomesha vitendo hivi kwenye jamii,” amesema Lilian.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa UTPC Keneth
Simbaya amesema kuwa vitendo vya ukatili wa kijisia hasa kwa wanawake na watoto
ni miongoni mwa ukiukwaji mkubwa uliokithiri wa haki za binadamu na kuwataka
wanahabari kushiriki vyema katika kuielimisha jamii.
Amesema kuwa vyombo vya habari vina nguvu na kubwa sana
ya kuifanya jamii kupata mambo ya kujadili, ambapo amewaomba waandishi wa
Habari kutumia kampeini hiyo kuifanya jamii ipate cha kujadili kuhusu masuala
ya ukatili wa kijinsia na kuyapinga.
"Waandishi wa habari kemeeni vitendo vya ukatili
kwa kuandika na kuibua kila aina ya vitendo vinavyosababisha ukatili, na sii
hivyo tu badala yake pia iwe sanjari na kutoa elimu kwa kuandaa vipindi pamoja
na kuzipa habari zihusuzo ukatili katika vyombo vyetu vya habari". Amesema
mkurugenzi.
Naye Afisa Programu, utawala na maendeleo ya Klabu Hilda
Kileo amesema Kupitia kampeni hiyo, UTPC itatumia siku16 katika kutoa elimu
ikiwemo kuandaa mada na mijadala mbalimbali ikiwemo ndoa na mimba za utotoni,
ukeketaji na vitendo vingine kama hivyo ambavyo vimekuwa na madhara makubwa na
wakati mwingine hata kugharimu maisha ya watu.
Hilda amesema kuwa Kwa mwaka huu kauli mbiu ya Kampeni
ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ni Wekeza, zuia ukatili wa kijinsia.
MWISHO.

Post a Comment