Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu kimeitaka serikali kutowapa tenda za ujenzi wa miradi ya maendeleo Wakandarasi weazembe na wanaokwamisha utekelezaji wa miradi.
Aidha, CCM imewataka watendaji wa serikali na wakandarasi kuhakikisha wanatekeleza miradi ya maendeleo kwa kuzingatia ubora na viwango ili kuleta thamani ya fedha.
Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohammed akiwa na Kamati ya Siasa ya Mkoa huo, mara baada ya kukagua ujenzi wa shule ya Sekondari Dakama unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi mil. 584.
Shemsa amemataka Mkuu wa Mkoa huo Dk. Yahaya Nawanda kutowapa kazi wakandarasi ambao hawatekelezi kwa wakati kwa sababu wanakwamisha jitihada za serikali ya Rais Samia.
‘’Wazabuni ambao wanapewa na lakini hawakamilishi kwa wakati, naomba wasipewe kazi awe ni kiongozi wa CCM au wa serikali, kama anakwamisha asipewe kazi…sababu hao ndio wanatufanya turudi nyuma’’ amesema Shemsa.
Aidha amempongeza Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha za kujenga shule mpya ya Dakama ili kutimiza adhma yake ya kutoa elimu bila malipo.
Amewataka wananchi wa Katan ya Dakama kumuunga mkono Rais Samia pamoja na serikali ya CCM, huku akimtaka Mkuu wa Mkoa kuhakikisha shule hiyo inapata maji kabla ya kuanza kutumia mwezi Januari 2024.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda amemhakikisha Mwenyekiti huyo wanazingatia maelekezo yaliyotolewa na CCM ikiwemo kusogeza huduma ya maji katika shule hiyo.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa shule hiyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwandete Fransisco Bujiku ambaye ni Msimamizi wa ujenzi wa shule hiyo amesema wanatekeleza mradi wa SEQUIP kwa gharama ya shilingi mil. 584.
Amesema lengo la mradi huo ni kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili kutoa elimu bora kwa wanafunzi ambapo mradi huo una vyumba nane vya madarasa, ofisi mbili, jengo la utawala, chumba cya TEHAMA, Maktaba, Maabara ya Fizikia, Baiolojia, Kemia, Matundu 04 ya vyoo vya wavulana na 04 ya wasichana, tenki la maji na vichomea taka viwili.
MWISHO.
Post a Comment