Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.
WAKAZI zaidi ya 6000 kutoka vijiji vitatu vya Kadoto, Malekano na Mwang’handa wilayani Maswa Mkoani Simiyu wanatarajia kunufaika na Mradi wa Maji unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi Mil. 718.6.
Wakizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya Kamati ya Siasa ya Mkoa huo kutembelea mradi wa Maji, wakazi wa vijiji hivyo waliipongeza serikali kwa kuwasogezea huduma ya maji karibu na makazi yao.
Maria Lucas, mkazi wa Mwang’handa alisema anaishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea mradi wa maji ambao umewapunguzia adha ya kutafuta maji umbali mrefu.
‘’Namshukuru sana Rais wetu Samia kwa kutuletea Maji, walifika wakaomba hili eneo hili ili wajenge mradi wa Maji, niliwapa na wakaniahidi kunipa maji na nimepata…nawashukuru sana viongozi wa serikali kwa kutujengea mradi wa Maji’’ alisema.
Rebeka James, Mkazi wa Malekano aliipongeza serikali kwa kuwasogezea huduma ya maji na kuwatua akina mama ndoo kichwani kwani hapo awali walikuwa wanafuata huduma ya maji mtoni na kutembea zaidi ya saa moja.
Akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Lucas Madaha alisema mradi huo unalenga kuhudumia wakazi wa vijiji vitatu vya Kadoto, Mwang’handa na Malekano.
Alifafanua kuwa kutokana na usanifu, mradu huo ulilenga kuhudumia watu 6,251 kutoka vituo 12 vya kuchotea maji, lakini ukikamilika utahudumia watu 4,000 kutoka vituo vinane vinavyojengwa.
‘’vituo vinne vilivyopunguzwa kutokana na gharama za mradi zilizowasilishwa na wakandarasi kuwa juu, tumefikia makubaliana kuwa vitajengwa mara baada ya mkandarasi kukamilisha kazi alizopewa’’ alisema Mhandisi Madaha.
Katibu wa CCM, Mkoa wa Simiyu Eva Ndegeleki aliipongeza serikali chini ya Rais Samia kwa kuleta fedha za miundombinu ya maji ili kutekeleza adhima ya kumtua mama ndoo kichwani.
Aliwaomba viongozi wa serikali zikiwemo kamati za siasa za tawi, kata na wilaya kuhakikisha wanawashawishi wananchi kuunganisha maji katika makazi yao kwa kulipia fedha kidogokidogo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohammed aliipongeza serikali na timu ya wilaya kuhakikisha miradi ya kumtua mama ndoo kichwani inakamilika.
Alisema Rais Dk. Samia ametekeleza miradi mingi ya Maji katika mkoa wa Simiyu huku akiwataka watendaji wa RUWASA wilaya ya Maswa kuhakikishia wanawasogezea wananchi huduma ya Maji katika awamu ya pili.
‘’Lengo la CCM na serikali iliyopo madarakani siyo tu kuweka miundombinu ya Maji bali tunataka maji yafike kwa wananchi…kupitia Ilani tuliwahakikishia maji yanafika kwenye nyumba, kupitia miradi hii Chama kitafurahi kuona maji yanafika majumbani’’ alisema Shemsa.
Aliwataka Watendaji wa RUWASA kuweka bei ambazo watazimudu ili wananchi wengi wapate maji na wanufaike na matunda ya Dk. Samia Suluhu Hassan.
Katika hatua nyingine, Kamati hiyo imeridhishwa na ujenzi wa shule mpya ya Msingi Butalo yenye mikondo miwili iliyopo kijiji cha Jija wilayani Maswa yenye thamani ya shilingi mil. 540.3.
MWISHO.

إرسال تعليق