Mkuu wa Wilaya ya Maswa
Mkoani Simiyu Aswege Kaminyoge, akizungumza na wajumbe wa Baraza la Biashara la
Wilaya hiyo wakati wa uzinduzi wake. |
Na Derick Milton, Maswa.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Aswege Kaminyoge ameitaka Ofisi ya
Biashara katika Halmashauri ya Wilaya hiyo, kazi yao ya kwanza iwe ni kutoa
elimu kwa wafanyabiashara ili biashara zao ziweze kukua.
Alisema kuwa kazi ya kwanza ya Afisa Biashara isiwe kukusanya ushuru au
kutoa leseni pekee kwa wafanyabiashara, bali iwe kuhakikisha Biashara zinakua
mara kwa mara.
Kaminyoge ametoa rai hiyo jana, wakati akizundua Baraza la Biashara la
Wilaya hiyo, ambapo ameeleza wafanyabishara wengi bado wanahitaji elimu katika
ufanyaji wa biashara zao.
“ Katika mwongozo wa Mabaraza,
unatutaka serikali kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabishara, niwatake
maafisa Biashara, kazi yetu ya kwanza iwe Elimu na siyo kukusanya ushuru pekee
au kutoa leseni...kazi ya leseni itakuja baadaye,” Alisema Kaminyoge.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya aliwahakikishia wafanyabiashara katika Wilaya
hiyo kuwa serikali itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo
kupunguza utitiri wa kodi ili waweze kufanya shughuli zao kwa amani.
Mratibu wa Mabaraza ya Wilaya na Mikoa kutoka Baraza la Biashara Taifa
(TNBC) Marco Chacha akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza hilo, alisema kuwa
lengo la uwepo wa Mabaraza ni kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabishara.
Chacha alisema kuwa Baraza la Biashara limeanzishwa kisheria, hivyo
linatakiwa kutumika kama jukwaa la kukwamua uchumi katika ngazi mbalimbali na
wafanyabiashara kuwasilisha hoja zao kwa serikali.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara katika Wilaya hiyo Winfrida Nige alisema
kuwa kilio kikubwa cha wafanyabiashara ndani ya Wilaya hiyo, kilikuwa ni juu ya
uanzishwaji wa Baraza hilo ili waweze kuwasilisha changamoto zao.
“ Tunaishukuru sana serikali kwa mara kwanza ndani ya miaka zaidi ya
mitatu leo Maswa tunapata Baraza, tunajua hili ndilo jukwaa letu la kutatuliwa
changamoto tunazokutana nazo kwenye kazi etu,” alisema Nige.
MWISHO.
إرسال تعليق