Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC,Mbunge, Stanslaus Mabula (aliye kati
mbele) akizungumza na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Paul
Maige (wa pili kulia) mara baada ya kukagua jengo la wagonjwa wa dharula
ktk Hospitali ya wilaya ya Maswa. Moja ya mitambo katika kiwanda cha Chaki kinachomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Na Samwel Mwanga, Maswa.
HALMASHAURI ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imepongezwa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kwa utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kutengeneza chaki na kuzitaka halmashauri nyingine kuiga mfano huo.
Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Stanslaus Mabula (Mb) Machi 26 mwaka huu wamefanya ziara ya ukaguzi wa miradi miwili ya maendeleo ambayo imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa katika halmashauri hiyo ikiwemo Ujenzi wa kiwanda cha Chaki na Jengo la wagonjwa wa dharura katika Hospitali ya wilaya hiyo.
Kamati ya LAAC imetoa pongezi kwa Madiwani pamoja na wataalam kwa kubuni wazo zuri la kuanzisha mradi wa kimkakati wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha Chaki ambacho kitakuwa ni chanzo cha mapato ya halmashauri hiyo na pia kitatoa fursa kwa wananchi wa wilaya hiyo kupata ajira.
“Nami niwapongeze sana kwa ujenzi huu wa kiwanda cha Chaki huu ni moja ya mradi wa kipekee wa kimkakati na kamati mara nyingi imekuwa ikisema halmashauri nyingi zinatamani kujenga stendi, masoko na vitu vingine vya namna hiyo lakini halmashauri ya wilaya ya Maswa kulingana na eneo lenu lilivyo,kulingana na malighafi ambayo mnaweza kuipata maeneo jirani mmebuni mradi mzuri sana wa kiwanda hiki,” amesema na kuongeza.
“Mradi ni mzuri sana na kamati inapenda kutoa wito kwa halmashauri zote nchini kupitia halmashauri ya wilaya ya Maswa kuwa wabunifu na kufikiria miradi mbadala ambayo itakuwa na uzalishaji bora itakayokuwa inatoa ajira na siyo ajira siyo za ndani tu hata nje kutokana na kuwawasaidia wengine na mradi huu utakapoanza mtaweza kuuza chaki nchi nzima na niendelee kusisitiza halmashauri ya wilaya ya Maswa ni mfano wa kuigwa,”amesema Stanslaus Mabula.
Wajumbe wa Kamati hiyo wametoa agizo kwa halmashauri hiyo kuhakikisha kiwanda hicho kinaanza uzalishaji ifikapo Mei 15 mwaka huu ili thamani ya fedha ya serikali iliyowekezwa katika kiwanda hicho.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wengine, Suma Fyandomo (Mb) mara baada ya kutembelea jengo la wagonjwa wa dharula katika hospitali ya wilaya hiyo amesema kuwa wameridhishwa na ujenzi wa jengo hilo ambalo thamani ya fedha imeonekana.
Amesema kuwa jambo jingine la kufurahisha ni vifaa vilivyoko kwenye jengo hilo ambavyo ni vya kisasa kwa ajili ya kumhudumia mgonjwa tofauti ya vifaa vya zamani huku akitolea mfano kuwa zamani mgonjwa alipokuwa akiongezewa hewa ya oksijeni alikuwa akilala na mtungi wa gesi kitandani lakini kwa njia ya kisasa mitungi iko chumba cha nje huku mgonjwa akiendelea kupatiwa huduma katika chumba maalum.
Aidha amewashauri wataalam wote kutunza vifaa vilivyoko katika jengo hilo pamoja na kutunza jengo hilo na miundombinu yake ambalo limejengwa kwa kiwango chenye ubora wa hali ya juu na linatoa taswira nzuri katika hospitali hiyo.
Awali Afisa Mipango kutoka Halmashauri ya wilaya hiyo, Ntobi Lufunga akitoa taarifa fupi ya kiwanda cha hicho kwa wajumbe hao amesema kuwa katika kipindi cha bajeti ya mwaka 2018/2019 halmashauri ya wilaya ya Maswa ilikuwa ni miongoni mwa halmashauri 17 hapa nchini ambayo ilipatiwa fedha kwa ajili ya kuendesha miradi ya kimkakati na wanatekeleza miradi miwili ukiwemo wa kiwanda cha chaki na kiwanda cha vifungashio na hadi sasa kiwanda hicho cha Chaki kimetumia gharama ya Shilingi Bilioni 10.16 hadi sasa.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa, Dr. James Bwire amesema kuwa jengo hilo la dharula kwa wagonjwa katika hospitali hiyo lilikamilika ujenzi wake mwaka Mwezi Julai mwaka 2021 na likaanza kutoa huduma Mwezi Machi mwaka 2022 baada ya vifaa vyote kukamilika vinavyotakiwa katika katika jengo hilo.
Amesema kuwa jengo hilo lina uwezo wa kuhudumia wagonjwa wa dharula 450 kwa mwaka lakini tangu lianzishwe hadi sasa limeweza kuhudumia wagonjwa 587 sawa na wagonjwa 54 wa dharula kwa mwezi na jengo hilo limekuwa msaada kwao kutokana na kuwa na vifaa vya kisasa na hivyo imewapunguzia gharama ya kusafirisha wagonjwa kwenda katika hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza kwani kwa sasa wanapatiwa matibabu hapohapo na wataalam wamewezeshwa kwa ajili ya kutoa matibabu hayo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Paul Maige ametoa shukrani za dhati kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiwezesha halmashauri hiyo kuipatia fedha za miradi mbalimbali ikiwemo miradi hiyo ambayo imetembelewa na wajumbe wa kamati hiyo.
“Nichukue fursa hii kumpongeza Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuletea fedha nyingi katika halmashauri yetu ambayo tunatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo hii miradi ambayo imetembelewa na kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa,”amesema.
MWISHO.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Maswa, Dk James Bwire (kushoto)
akisoma taarifa ya jengo la wagonjwa wa dharula kwa Makamu Mwenyekiti
Kamati ya LAAC, Mbunge Stanslaus Mabula (wa kwanza kulia).
Afisa Mipango halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Ntobi Lufunga (kushoto) akitoa taarifa ya kiwanda Cha Chaki kwa wajumbe wa LAAC .
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com




إرسال تعليق