Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu David Masanja akiongea kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Bariadi limeitaka Bodi ya Pamba nchini (TCB) kuhakikisha linahudumia wakulima kwa wakati badala ya kuwageuza mtaji kwa kutowapatia pembejeo na kukusanya fedha bila kuwahudumia wakulima hao.
Hayo yamebainishwa Mwishoni mwa wiki jana, kwenye kikao cha Kujadili taarifa za robo ya pili ya Maendeleo ya Halmashauri hiyo ambapo walihoji Wakulima wa Pamba hawapati pembejeo kwa wakati, huku wakulima wa mazao mengine ambao hawapatiwi pembejeo lakini wanaweza kujihudumia.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo David Masanja aliitaka Bodi ya Pamba kukaa na wakulima wa pamba ili kuweza kubaini changamoto na mahitaji yao kuliko kuletewa pembejeo muda ambao wakulima hawazihitaji.
‘’Wameshindwa kutoa pembejeo na viuatilifu kwa wakati, kwa nini wakulima wa alizeti, mahindi, choroko, dengu na mpunga wanajinunulia pembejeo na hawana makato?...Bodi ya Pamba tuna ajenda na nyinyi.’’ Alisisitiza Masanja.
Aliongeza kuwa wakulima wa pamba wanalazimishwa kukatwa fedha kwa ajili ya kulipia pembejeo wakati wa mauzo hata kama hawakuchukua fedha bila kujali idadi ya pembejeo walizopata.
Alisema wakulima wa pamba wamekuwa wakipatia chupa za dawa bila kuzingatia idadi ya ekari, lakini pia hazitoshelezi mahitaji huku wengine wakilazimika kugawiana jambo ambalo amesema haliwezekani.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Martine Singibala alisema kwenye kata yake ya Mhango, Bodi ya Pamba imegawa chupa za dawa ambazo hazitoshelezi mahitaji huku akiwataka Maafisa kilimo kufuatilia hali hiyo.
Diwani wa kata ya Guduwi Nhandi Mnyumba alisema katika kata yake wamepatiwa pembejeo kidogo ambazo hazitoshelezi mahitaji ya wakulima huku wakishindwa kuzigawanya kwa wakulima.
Diwani wa Kata ya Nyangokolwa Nkenyenge Charles alisema suala la pamba ni muhimu kwa sababu linagusa uchumi wa Bariadi na Mkoa wa Simiyu ambapo aliwataka madiwani kuweka adhimio na mkakati maalumu juu ya usimamizi wa zao la pamba.
Alisema viongozi wanashindwa kuhamasisha kilimo cha pamba kutokana na uhaba wa pembejeo, lakini wakulima wamekuwa wakikatwa fedha wakati wa mauzo kutokana na kupatiwa pembejeo ambazo zimekuwa hazitoshelezi mahitaji.
‘’Sisi kama madiwani tunatakiwa tuwe msitari wa mbele kuwapigia kelele wakulima wetu ili waweze kupata haki yao, wataalamu wa kilimo watusaidie kuhakikisha pembejeo zinafika kwa wakati…vinginevyo wakulima waruhusiwe kujinunuliwa wenyewe’’ alisema Nkenyenge.
Awali akitoa ufafanuzi, Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo na Mifugo Dk. Linah Andrea alisema wakulima wamepata changamoto za mvua nyingi wakati wa kupulizia jambo ambalo limesababisha pembejeo kutowafikia wakulima kwa wakati.
Alisema hadi sasa Bodi ya Pamba imetoa ekapaki (chupa) 83,920 kwa ajili ya kusambaza kwa wakulima lakini pia wameomba nyongeza ya ekapaki 36,000 kwa jili ya kuwapatia wakulima wa Pamba.
MWISHO.
Waandishi wa vikao (CC) wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Bariadi wakiwa kwenye mkutano wa Baraza la Madiwani.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Issa Mtweve akichangia hoja kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.




إرسال تعليق