CCM yaonya Watumishi wa Afya Itilima.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohammed akisisitiza jambo kwenye mkutano wa Tarafa kwa Tarafa uliofanyika kata ya Laini Wilayani Itilima.


Na COSTANTINE MATHIAS, Itilima.

 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu kimewaonya watumishi wa Afya Wilayani Itilima, Mkoani humo kuhakikisha wanatoa huduma bora ili wananchi waone matunda ya serikali ya CCM.

 

Aidha wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuacha mazoea ili kuondoa changamoto na malalamiko kwa wananchi juu ya ukosefu wa huduma kwenye Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali.

 

Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo Shemsa Mohammed wakati akiongea na viongozi wa matawi, mashina na kata za Tarafa ya Bumera kwenye zaira yake ya Tarafa kwa Tarafa inayoendelea kwa lengo la kuimarisha na kukagua uhai wa chama.

 

Amesema Ilani ya CCM ambayo wamefunga mkataba na wananchi 2020/2025 wakati wakiomba kura iliekeza watoto, wazee na wakina mama wajawazito wakapate huduma bure kwenye huduma za afya.

 

‘’Ninasikitika kuona wazee hawapewi huduma Itilima na wakina mama wanalipishwa kadi za kliniki, Mkuu wa wilaya najua umelipokea utalifanyia kazi…awamu nyingine nisisikie kero za wakina mama kulipisha kadi za kliniki, Wizara ya Afya inaelekeza ni bure’’ amesema.

 

Ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia anataka na kuelekeza huduma zifike kwa wananchi kama inavyopaswa na siyo kulipisha wazee na wakinamama wajawazito.

 

‘’Kwenye Mkoa wa Simiyu, mtumishi ambaye hawezi kutimiza wajibu wake wa kuhudumia wananchi anaacha wanajifungulia kwenye sakafu kwa shida zake binafsi, hatufai kwenye mkoa wetu…lengo la zahanati na kituo cha afya ni kuwapatia wananchi huduma bora’’ amesema.

 

Wakizungumza wakati wa kuwasilisha kero zao, baadhi ya wananchi wamesema wanawake wajawazito wanapata shida kwenye zanahati wakati wa kujifungua ikiwemo kuombwa fedha za kununua kadi za kliniki.

 

Samwel Mbabani mkazi wa Sagata amesema wauguzi hawatoi huduma nyakati za usiku ikitokea mama mjamzito amekwenda kujifungua.

 

Ameongeza kuwa wamekuwa wakiomba shilingi elfu tano kwa ajili ya kadi la kliniki kwa watoto jambo siyo maelekezo ya serikali kupitia Ilani ya CCM.

 

Kaimu Mwenyekiti wa Wazee Kijiji cha Laini Masumbuko Langa ameimboa serikali kusimamia maekeleza juu ya utoaji wa huduma bure.

 

Kaimu Mganga Mkuu wilaya ya Itilima Oswin Mlelwa amewaelekeza watumishi wa afya kuhakikisha wanatoa huduma muda wote ili wananchi waweze kupata huduma katika maeneo hayo.

 

Kuhusu kero ya wazee, Oswin amesema wazee wote wenye umri zaidi ya miaka 60 wanatakiwa kupata huduma bure lakini wazee wengi wanakwenda kwenye huduma bila barua za msamaha wa matibabu.

 

‘’Viongozi wa vijiji na kata watambueni wazee wanaostahili kupata matibabu bure, waandikieni barua za msamaha ili wakienda kupata huduma waweze kutibiwa bure…wazee nendeni mkapate huduma na zingatieni taratibu ili mpate huduma’’ amesema Oswin.

 

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Itilima Anna Gidarya amekiri kuwepo kwa watoa huduma wa afya wenye changamoto licha ya juhudi za serikali kuboresha miundombinu ya afya.

 

‘’Nimeshaongea na Mganga Mkuu wa wilaya, aniletee orodha ya wasiotekeleza wajibu kwa wananchi ili nilinganishe na upande wangu…ugonjwa hauchagui saa wala siku, ‘’ amesema.

 

MWISHO.

 

 

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohammed (mwenye miwani) akisalimia na viongozi wa mashina, matawi na kata za Tarafa ya Bumela wilayani Itilima mkoani humo.


Wananchi wa Tarafa ya Bumera wakiwa kwenye mkutano.

 

Mwenyekiti wa CCM Mkoa Shemsa Mohammed (katikati) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kufika kwenye mkutano wa Tarafa kwa Tarafa uliofanyika kata ya Laini, kulia ni Kaimu Katibu ws CCM Mkoa wa Simiyu Naboth Manyonyi, kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Itilima Mhuli Ngeleja.
 
 
Mkuu wa Wilaya ya Itilima Anna Gidarya akizungumza kwenye mkutano uliofanyika Laini Sekondari.
 


Wananchi wa Tarafa ya Bumera wakiwa kwenye mkutano.

 



Wananchi wa Tarafa ya Bumera wakiwa kwenye mkutano.



 

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم