Wafanyabiashara wa Mbao walia gharama za kushushia mizigo Kidulya.

 

Wafanya biashara wa Mazao ya Misitu katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi.


Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

 

WAFANYABIASHARA wa Mazao ya Misitu katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu wamelalamikia kitendo cha kuzuiwa kushusha mbao kwenye biashara zao na badala yake washushe na kupakia kwenye magari madogo katika maegesho yaliyoko nje kidogo ya mji eneo la Kidulya, hali inayowasababishia harasa na kulipa ushuru mara mbili.

 

Wakizungumzia adha hiyo wamesema wamekwama kuhudumia wananchi hali iliyowasababisha kufunga biashara zao kutokana na kutopata faida licha ya kulipa kodi na ushuru wa serikali.

 

Membi Ngasani ambaye ni mfanyabiashara wa mazao ya misitu amesema wameshindwa kuhudumia wananchi huku wakiiomba serikali kuwaruhusu kushushia katika maeneo yao ili wahudumia wananchi pia walipe kodi za serikali.

 

John William, mkazi wa Bariadi amesema ameshindwa kusafirisha mbao kutokana na gharama za kushusha na kupakia kwenye magari madogo hali inayowasababishia hasara kubwa.

 

‘’leo ni miezi mitatu sijaleta mbao kutokana na gharama za kushusha na kupakia, takribani 800,000 nalipa ili kufikisha mzigo wangu sehemu husika…tunamwomba Mkuu wa Mkoa au Rais Samia asikie kilio chetu tushushe kwenye biashara zetu’’ amesema William.

 

Sungwa Mongo, mfanyabiashara wa mazao ya Misitu amesema wanatumia gharama kubwa kushusha mbao kutoka Kidulya hadi kwenye maeneo yao hali inayowasababishia hasara na kushindwa kufanya biashara.

 

Mwenyekiti wa Wafanyabishara John Sabu amekiri kuwepo kwa adha hiyo na kusababisha sintofahamu kwa wafanyabiashara wa mbao jambo ambalo linawasababishia hasara na kupandisha bidhaa ili kufidia hasara inayojitokeza.

 

Ameiomba serikali kurejesha mfumo uliokuwa unatumika awali wa kushushia mbao mjini wakati huo magari yaruhusiwe kuingiakwenye maegesho kwa ajili ya kulipa ushuru wa serikali.

 

Akizungumzia kero hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Adrian Jungu amesema Halmashauri hiyo imeweka utaratibu wa malori yote yanayozidi tani kumi kushusha mizigo eneo la Maegesho Kidulya ili kuzilinda barabara za mjini zilizotengenezwa kwa gharama kubwa.

 

Ameongeza kuwa Halmashauri hiyo wanaendelea kuimarisha ulinzi katika eneo hilo pamoja na kupima viwanja ili wananchi waweze kujenga na kuboresha huduma za kijamii.

 

MWISHO.

 

Loli likishusha mbao katika maegesho ya Magari yaliyoko mtaa wa Kidulya katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.


Zoezi la Kupakua mbao kwenye lori kubwa na kupakia kwenye gari ndogo likiendelea katika maegesho ya magari mtaa wa Kidulya.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Adrian Jungu akitoa ufafanuzi juu ya zuio la wafanyabiashara wa mbao kutoshusha mjini.


Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Simiyu John Sabo akizungumzia zuio la wafanyabishara wa mbao kutoshushia mjini.


Wafanyabishara wa mbao wakiwa wamekaa katika sehemu za biashara zao.


 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم