Mbunge wa Jimbo la Bariadi, Mhandisi Kundo Mathew amesema kwamba Jimbo la Bariadi litaendelea kuwa ngome imara ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhandisi Kundo amesema wananchi wa Bariadi wanatambua juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita katika kuboresha huduma za jamii, ikiwemo Elimu, Afya, Miuundombinu, Maji, na Umeme.
Amebainisha kuwa miradi ya maendeleo imewagusa wananchi wa kila kata, jambo linalothibitisha dhamira ya CCM kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa vitendo.
"Leo hii tunashuhudia maendeleo makubwa katika kila sekta hapa Bariadi. Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeleta miradi mikubwa ya barabara, shule, hospitali, maji safi na salama, na umeme, jambo ambalo limeifanya Bariadi kuwa mfano wa utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo,” amesema Mhandisi Kundo.
Aidha, Mbunge huyo alimhakikishia Makamu Mwenyekiti wa CCM kuwa wananchi wa Bariadi wamejipanga kuhakikisha chama kinapata ushindi mkubwa katika uchaguzi ujao wa Oktoba, akisisitiza kuwa jimbo hilo litaandika historia kwa kupata kura za mafuriko.
“Tuna imani kubwa na chama chetu na tunatambua kazi nzuri inayofanywa na serikali...hakuna shaka kwamba Bariadi itaendelea kuwa ngome ya CCM na ushindi wetu utakuwa wa kishindo,” ameongeza.
Aidha, ziara hiyo ya Makamu Mwenyekiti wa CCM imeongeza hamasa kwa wanachama na wananchi kwa ujumla, huku viongozi wa chama wakisisitiza umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi ujao.
Wananchi wa Bariadi wamethibitisha kuwa wataendelea kuwa sehemu ya historia ya ushindi wa CCM kwa kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kupiga kura mwezi Oktoba.
Mwisho.
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Steven Wasira akiwa kwenye Mkutano wa hadhara Jimbo la Bariadi, uliofanyika katika Kijiji cha Ngulyati wilayani Bariadi.

Post a Comment