RC KIHONGOSI AKEMEA FITINA, MAJUNGU NA CHUKI MAHALA PA KAZI

 

Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenan Kihongosi akihutubia wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya wafanyakazi mkoa wa Simiyu iliyofanyika wilaya ya Maswa.


Samwel Mwanga, Maswa


MKUU wa mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi, amewataka watumishi wa umma mkoani humo kuachana na tabia za fitina, majungu na chuki katika maeneo ya kazi, akisisitiza kuwa hali hiyo inachangia kuporomoka kwa tija na kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.


Akizungumza leo Mei Mosi,2025, wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Nguzonane wilaya ya Maswa, amesema vitendo hivyo vimekuwa vikiwanyima watumishi morali ya kazi na kuvuruga mshikamano unaohitajika ili kufanikisha malengo ya serikali.


Amesema kuwa katika baadhi ya halmashauri na idara za serikali,hali hii imewahi kusababisha hata kusambaratika kwa timu za usimamizi au kushindwa kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo kutokana na kutokuwepo kwa mshikamano.


"Tujenge upendo na mshikamano miongoni mwetu. majungu, chuki na fitina vinaua morali ya kazi na vinarudisha nyuma jitihada za maendeleo,serikali inahitaji watu wanaofanya kazi kwa moyo mmoja," amesema.

Aliongeza kuwa,watumishi wanaoweka mbele maslahi binafsi kwa kutumia njia za kudhalilisha wenzao hawawezi kujenga taasisi imara, bali huchangia migogoro isiyo ya lazima kazini.


Pia amewataka viongozi wanaoongoza taasisi za serikali kuhakikisha wanazitumia vizuri kwa kutoa huduma kwa wananchi sambamba na kuwasimamia walio chini yao kwa kufuata taratibu zilizowekwa na siyo kuwanyanyasa.


“Nawahimiza viongozi wa taasisi hasa za serikali kuwa mfano wa kuigwa kwa kuhimiza maadili ya kazi, uwazi na mawasiliano bora baina ya wafanyakazi walioko chini yenu,”amesema.


Elias John ni mwanachama wa Chama Cha Walimu Tanzania(CWT)amesema kuwa taasisi nyingi za serikali kwa sasa zinapambana na mahusiano duni kazini jambo ambalo linaathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.


 “Kauli ya Mkuu wa Mkoa imekuja wakati muafaka ambapo taasisi nyingi za serikali zinapambana na changamoto ya mahusiano duni kazini, jambo linaloathiri ufanisi wa huduma kwa wananchi,:amesema.


Naye Elias Maduhu ambaye ni mwanachama wa Chama Cha wafanyakazi wa Serikali za Mitaa(TALGWU)amesema kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watumishi kuwa njia zisizo rasmi kama kumchafua mwingine kwa maneno ndizo zinazotumiwa na baadhi ya watu kupanda vyeo.


“Hili linafifisha maadili ya kazi na kuwakatisha tamaa wale wanaojituma kwa uaminifu,wakati mwingine, viongozi huchukua hatua kwa misingi ya taarifa za majungu badala ya ukweli wa kitaaluma jambo ambalo si zuri,”amesema.


Awali, Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA)mkoa wa Simiyu,Lucy Masegenya akisoma taarifa ya shirikisho hilo amesema kuwa wapo baadhi ya maafisa utumishi katika halmashauri za wilaya mkoani humo wamekuwa wakishindwa kutoa ushirikiano na maelekezo kwa watumishi wa serikali wanapofika katika ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri kuwasilisha changamoto zao za kazi.


“Mheshimiwa mgeni rasmi katika mkoa wetu wa Simiyu moja ya changamoto wanazozipata watumishi wa serikali ambao wako chini ya Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na Mji ni baadhi ya maafisa utumishi katika halmashauri hizo kushindwa kuwapatia ushirikiano pindi wanapofika katika halmashauri hizo kutokana na shida mbalimbali za kikazi,”amesema.


Katika kuadhimisha siku hiyo watumishi hodari kutoka katika vyama mbalimbali vya wafanyakazi walitunukiwa zawadi mbalimbali zikiwemo vyeti,fedha,pikipiki na runinga.


Siku ya Mei Mosi ni jukwaa muhimu kwa wafanyakazi duniani kote kupaza sauti kuhusu masuala yanayowahusu, ikiwa ni pamoja na mazingira bora ya kazi, maslahi, na haki za msingi. Mwaka huu, kauli mbiu ya kitaifa ni "Mishahara Stahiki na Hifadhi ya Jamii kwa Wafanyakazi Wote ni Msingi wa Haki na Heshima Kazini."

MWISHO.


Mwl Neema Makundi (kushoto)akipokea cheti cha mfanyakazi hodari.


Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa akionesha cheti baada ya kuwa mfanyakazi hodari.


Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenan Kihongosi (kushoto) akimkabidhi Seti moja ya runinga,mfanyakazi hodari, Mhandisi Isaack Fimbo (kulia) Meneja wa Tanesco wilaya ya Maswa.


Katibu wa TUCTA mkoa wa Simiyu,Mwl Lucy Masegenya akisoma risala ya shirikisho hilo wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya wafanyakazi mkoa wa Simiyu iliyofanyika wilaya ya Maswa.


Sehemu ya wafanyakazi wa mkoa wa Simiyu wakifurahi wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani iliyofanyika mjini Maswa.


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post