
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
WANANCHI wa Kata ya Matongo, wilayani Bariadi Mkoani Simiyu, wamesifu Utendaji wa Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika Utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo imefungua fursa za uchumi na kukuza vipato vya wananchi.
Aidha, wananchi hao wameipongeza serikali kwa kujenga kituo cha kudhibiti Tembo waliokuwa wanavamia makazi yao na kuharibu mali za wananchi hao wanaoishi pembezoni mwa hifadhi ya Serengeti.
Akizungumza leo, kwenye mkutano maalumu wa kuwasilisha Ilani ya CCM, ulioandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Bariadi, Mhandisi Kundo Mathew, Diwani kata hiyo, Ng'hwani Edward ameipongeza pia serikali kwa kujenga kituo cha Afya Matongo ambacho kimerahisha upatikanaji wa huduma ya afya katika eneo hilo.
"Tunaipongeza serikali ya Rais Samia kwa kujenga kituo cha Afya Matongo, umeme upo, Barabara, Maji yapo, Mawasiliano ya simu na pia tumejengewa kituo cha kidhibiti Tembo, gari na askari wapo...tunaishukuru sana serikali, tunaomba watuongezee maskari ili wananchi hawa waishi kwa furaha" amesema Edward.
Mbunge wa Jimbo hilo, Mhandisi Kundo amesema ndani ya miaka mitano (2020/2025), kata ya Matongo imepatiwa zaidi ya shilingi Bil. 4.36 kwa ajili ya miradi ya Maendeleo tofauti na miaka mitano ya nyuma (2015/2020) ambapo ilipatiwa shilingi Mil. 233.
"Sekta ya Afya, tumejenga kituo cha Afya Matongo pamoja na zahanati ya Salalia...katika Uongozi wa Rais Dk. Samia hadi mwezi Disemba tutafikisha vituo vya afya vitano ambavyo ni Matongo, Miswaki, Ng'wang'wali na tunaenda kujenga Kilalo na Bunamhala, pia tumekabidhi Ambulance 1 Matongo" amesema Mhandisi Kundo.
Katika Sekta ya Maji, Mhandisi Kundo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji amesema serikali imekamilisha mradi wa maji Salalia kwa gharama ya shilingi Mil.553 pamoja na mradi wa Maji Matongo ambao umekimilika na unatoa maji kwa gharama ya shilingi Mil.560.
Kwenye sekta ya Elimu, amesema wamefanikisha kujenga shule ya msingi Madukani kwa zaidi ya shilingi Mil. 500 pia wamepatiwa shilingi Mil. 350 za kujenga mnara wa mawasiliano.
Kuhusu udhibiti wa Tembo, Mbunge huyo amesema wataendelea kupigana sababu Rais Dk.Samia amekuwa mama anayejali na kusikiliza wananchi.
"Ametupatia gari moja na askari, lakini bado tunaendelea kupambana ili kudhibiti tembo hao na tunamwomba atuongezee magari sababu bado wanatutesa, bila kutatua changamoto ya tembo Wana matongo hawataedelea kuzaliana" amesema.
Kwenye kata Matongo, Mbunge huyo amekabidhi mipira 19 kwa ajili ya vijiji vya Salalia, Matongo, Mwantimba na Ng'arita ambapo Kila Kijiji kimepata mipira minne na jezi pea 1 huku kata ya Matongo mipira mitatu na jezi pea moja pamoja na pampu Moja moja kwa kila Kijiji
Mwisho.
Post a Comment