SHILINGI BIL. 29 ZAPELEKA MAPINDUZI HUDUMA YA MAJI MASWA.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa Mhandisi Nandi Mathias akimtwisha ndoo mmoja wa wakazi wa kijiji cha Buyubi ikiwa ni sehemu ya kuzindua vituo vya kuchotea maji katika Kata ya Mwamashimba wilaya ya Maswa.


Na Samwel Mwanga, Maswa.


MAMLAKA  ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA) imetumia zaidi ya Shilingi Bil. 29 kukamilisha jumla ya miradi 18 ya maji safi na salama katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu.


Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya kutembelea miradi hiyo, Mkurugenzi wa MAUWASA, Mhandisi Nandi Mathias, amesema kiasi hicho cha fedha kimetolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa maeneo yanayohudumiwa na mamlaka hiyo.


Katika kijiji cha Buyubi, Kata ya Mwamashimba, Mhandisi Nandi amesema mradi mmoja kati ya hiyo 18 tayari umekamilika kwa gharama ya Sh bilioni 1.3 na unatarajiwa kunufaisha wakazi zaidi ya 16,000 katika vijiji vitatu vya Buyubi, Likungulyasubi na Dodoma.


"Mradi huu umeweka vituo 16 vya kuchotea maji pamoja na mabirika mawili kwa ajili ya mifugo, huku chanzo chake kikuu kikiwa ni bwawa la New Sola lililopo kijiji cha Zanzui hapa wilayani Maswa," amesema Mhandisi Nandi.


Aliongeza kuwa mbali na miradi ya ndani ya wilaya, mamlaka hiyo pia inasimamia utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria, unaoanzia Malampaka  wilayani humo Maswa hadi Malya  wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza.


Kwa mujibu wa Mhandisi Nandi, lengo kuu la miradi hiyo ni kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji salama kwa wananchi, hususan katika vijiji ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa vikitegemea maji kutoka vyanzo visivyo salama kama mito na mabwawa ya asili.


Kwa upande wao, baadhi ya wanufaika wa mradi huo waliipongeza serikali kwa kupeleka huduma ya maji karibu na makazi yao, wakisema imewasaidia kuokoa muda na kuongeza tija kwenye shughuli za kiuchumi.


"Awali tulitembea zaidi ya kilomita tano kufuata maji kwenye mito yenye mashaka ya usalama wa kiafya, lakini sasa tunapata maji karibu kabisa na nyumbani," amesema Yustina Deus, mkazi wa kijiji cha Buyubi.


Naye Buyaga Chai kutoka kijiji cha Likungulyasubi amesema: "Sasa wake zetu hawalazimiki tena kuamka alfajiri kusaka maji porini, tumeondokana na hali hiyo ya kinyama."


Veronika Moga, mkazi mwingine wa kijiji Buyubi, alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kumeondoa hatari ya kutumia maji kutoka kwenye visima vilivyokuwa vikitumiwa pia na wanyama pori kama fisi.


"Tulikuwa tunakutana na fisi wakinywa maji kwenye visima vya mtoni, lakini sasa tuna maji safi na salama hapa kijijini," amesema.


Miradi hii ni sehemu ya juhudi za serikali ya awamu ya sita kuhakikisha huduma za msingi zinawafikia wananchi vijijini, hasa maeneo yaliyokuwa yakikumbwa na changamoto ya maji kwa muda mrefu.


Mwisho.


Mhandisi Nandi Mathias aliyepo mbele akitoa maelezo mara ya kukamilika kwa kituo cha kuchotea maji katika kijiji cha Likungulayasubi wilaya ya Maswa.


Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Mhandisi Nandi Mathias akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya kukamilika kwa mradi wa maji katika Kata ya Mwamashimba wilaya ya Maswa.


Moja ya kituo cha kuchotea maji katika kijiji cha Buyubi kilichojengwa na Mauwasa.


Tenki la kuhifadhi lita 200,000 za maji lililojengwa na Mauwasa katika kijiji cha Buyubi wilaya ya Maswa.





Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post