UWEKEZAJI WA VIWANDA VYA NGS UVINZA, TANGANYIKA WAVUTIA WAKULIMA KUGEUKIA PAMBA.



Na Costantine Mathias, Kigoma/Katavi.


UWEKEZAJI mkubwa wa viwanda vya kuchambua pamba uliofanywa na Kampuni ya NGS katika wilaya za Uvinza (Kigoma) na Tanganyika (Katavi) umeleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kilimo kwa wananchi, hasa kwa kuhamasisha wakulima wengi kuachana na kilimo cha tumbaku na kuanza kulima pamba kwa wingi.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari, wakulima wa maeneo hayo wameeleza kuwa uwepo wa viwanda hivyo umeongeza hamasa ya kulima pamba kutokana na uhakika wa soko, elimu ya kilimo bora na mahitaji makubwa ya malighafi hiyo.



Saguda Sayi ambaye ni Mkulima kutoka Kijiji Cha Chakulu wilayani Uvinza amesema kuwa wakulima wengi wamegeukia kulima Pamba baada ya kuona jitihada za Serikali pamoja na uwekezaji wa Kampuni ya kuchambua Pamba ya NGS iliyoko wilayani Uvinza.


Afisa Uzalishaji kutoka kampuni ya NGS Uvinza, Baraka Kampala amesema kutokana na Uwekezaji huo, wakulima wanatakiwa kuzingatia maelekezo ya Maafisa Ugani ili kulinda ubora wa pamba. 



Magolanga Gervas, mkulima wa Kijiji cha Kapanga wilayani Tanganyika, anawataka wakulima kuzingatia ubora za Pamba na kufuata maelekezo ya Maafisa ugani ili kulinda Viwanda.


Afisa Kilimo wa Kampuni ya NGS wilayani Tanganyika amesema kuwa wanashirikiana na Maafisa Ugani wa BBT kuwaelimisha wakulima ili kuongeza tija ya uzalishaji na kupata mavuno ya kutosha wajikwamue kiuchumi.


Meneja wa Kiwanda cha kuchambua Pamba Cha NGS Tanganyika, Kashilila Mwita amesema kutokana na uwekezaji huo, wanafuata maelekezo ya serikali ikiwemo kuelimisha wakulima pamoja na kulinda ubora wa Pamba pindi inapofika kiwandani.


"Pamba ikifika kiwandani inatenganishwa madaraja wakati wa uchakataji ili kulinda ubora wa pamba mbegu zinazozalishwa...wakulima wengi walikuwa hawajui Kilimo cha pamba, lakini kutokana na uwepo wa Kiwanda tumepiga hatua katika uzalishaji" amesema.


Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Tanganyika , Focus Bugelaha amesema kuwa wakulima wameanza kubadilika kwani katika Msimu wa 2024 wakulima walikuwa wanaozalisha kilo 300 mpaka 500 lakini msimu wa 2025 wakulima wanaweza kupata kilo 800 mpaka 1500 kwa ekari moja.


"Mwaka jana tukipata kilo mil. 3.1 na Mwaka huu tunatarajia kupata zaidi ya kilo Mil. 7 kulingana na mwitikio wa wakulima kupata elimu" amesema.


Uwekezaji wa viwanda vya kuchakata pamba vya NGS katika wilaya za Uvinza na Tanganyika umeanza kuzaa matunda kwa kuongeza thamani ya pamba inayozalishwa, kuwapatia wakulima soko la uhakika na kuongeza ajira kwa vijana na wanawake vijijini.


Hii ni ishara njema kwa mikoa ya Kigoma na Katavi kuingia rasmi katika ramani ya mikoa inayotegemea pamba kama zao la biashara linaloweza kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wake.


Mwisho.









Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم