Wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Simiyu na Mara katika mafunzo ya usalama kwa wachimbaji wadogo wa madini na wadau wa sekta ya madini wa mikoa hiyo. (Picha na Derick Milton)
Na Derick Milton, Bariadi.
Tume ya Madini imewataka wachimbaji
wadogo wa madini kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na miongozo ya usalama
inayotolewa na wataalam wa sekta hiyo ili kukomesha ajali zinazoendelea
kuripotiwa katika maeneo ya uchimbaji.
Wito huo umetolewa leo na Kamishna
wa Tume ya Madini, Mhandisi Theonestina Mwasha, wakati wa ufunguzi wa mafunzo
ya usalama kwa wachimbaji wadogo wa madini na wadau wa sekta ya madini kutoka
mikoa ya Simiyu na Mara yaliyofanyika mjini Bariadi, mkoani Simiyu.
Mhandisi Mwasha amesema Serikali
kupitia Wizara ya Madini imejipanga kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia
elimu, vifaa na teknolojia ili kuwawezesha kujiinua kutoka katika uchimbaji wa
kiwango cha chini hadi kuwa wachimbaji wa kati na baadaye wakubwa.
“Lengo kuu la mafunzo haya ni
kuwaongezea uwezo wa kitaalam ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali
zinazoikumba sekta hii, hususan katika maeneo ya usalama migodini,” amesema
Kamishna Mwasha.
Aidha, amewataka wachimbaji hao
kuzingatia matumizi salama ya kemikali, hususan zebaki, kwa kuwa matumizi
mabaya yake yamesababisha madhara yasiyorekebishika kwa afya ya binadamu na
mazingira.
“Mafunzo haya yamejikita katika
sheria na kanuni za usalama mahali pa kazi pamoja na Sheria ya Madini. Ni
muhimu sana kuhakikisha mnafuata miongozo hii katika kutekeleza shughuli zenu,”
amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkaguzi Mkuu wa
Migodi kutoka Tume ya Madini, Mhandisi Hamis Kamando, amesema ajali nyingi
zinazotokea migodini husababishwa na kutokuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa
na mamlaka husika.
Amebainisha kuwa baadhi ya ajali
hizo zimesababisha vifo na ulemavu kwa wachimbaji, ambapo changamoto kubwa ni
kuanguka kwa miamba, kuteleza katika ngazi na ukosefu wa hewa safi ndani ya
maeneo ya uchimbaji.
“Ni wajibu wa kila msimamizi wa
mgodi kuhakikisha hatua zote za kiusalama zinafuatwa kikamilifu ili kuzuia
madhara haya,” ameongeza Mhandisi Kamando.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha
Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Simiyu, Mashauri Ntizu, ameishukuru Tume ya Madini
kwa kuandaa mafunzo hayo na kuyafikisha kwa wachimbaji wa mkoa huo.
“Mafunzo haya ni suluhisho la muda
mrefu kwa changamoto zinazowakabili wachimbaji. Kupitia semina hii tumejifunza
sheria, kanuni na mbinu bora za kufanya kazi kwa usalama,” amesema Ntizu.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwafikia
wachimbaji wadogo katika mikoa mingine nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa
Serikali wa kuboresha mazingira ya uchimbaji na kuimarisha mchango wa sekta ya
madini katika pato la taifa.
إرسال تعليق