Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
MKUU wa Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu Saimon Simalenga amewataka Wakandarasi wanaotekeleza Miradi ya Maji wilayani humo kuhakikisha wanatekeleza kwa Viwango, Ubora na kuzingatia muda wa Mkataba.
Amesema serikali haitawavumilia wakandarasi wazembe na kwamba haitawaongezea siku baada ya muda wa utekelezaji kukamilika, huku akiwataka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) kuendelea kuwasimamia wakandarasi ili watekeleze kwa mujibu wa Mkataba.
Simalenga ameyasema hayo wakati akikagua miradi ya maji inayotekelezwa katika vijiji vya Gasuma, Byuna, Matongo, Ibulyu, Igegu, na mtaa wa Old Maswa mjini Bariadi.
Amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuleta fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji ili iweze kuwanufaisha wananchi kwa kuwasogezea huduma ya maji.
Simalenga amezitaka Kamati za maendeleo za vijiji na kata kuhakikisha wanakagua na kusimamia ujenzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye vijiji vyao.
‘’Tutunze miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yetu, huduma ya maji inahitaji gharama kidogo kuchangia, baada ya mradi kukamilika tuchangie gharama za maji ili tuendelee kupata huduma za Maji…viongozi wa CCM muwe wa kwanza kuelimisha wananchi’’ amesema Simalenga.
Amewataka wananchi kulinda na kutunza vyanzo vya maji pamoja na miradi inayoletwa na serikali ambapo miradi hiyo inaletwa kutokana ana kuwepo kwa viongozi bora wakiwemo wenyeviti wa vijiji, madiwani, Mbunge pamoja na Rais.
‘’nitapita kukagua, nataka nione miradi hii inatekelezwa kwa viwango, ubora na kuzingatia muda wa mkataba, hatutamwongezea muda mkandarasi baada ya muda mkataba kumalizikia’’ ameonya Simalenga.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya amewataka viongozi wa Vijiji kufanya mikutano ya hadhara ili kukutana na wananchi kila baada ya miezi mitatu ili wawasomee mapato na matumizi ikiwemo miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) wilaya ya Bariadi Mhandisi Emmanuel Luswetula amesema miradi wa maji Byuna unatekelezwa kwa gharama ya shilingi mil. 462.
Amesema mradi huo unatekelezwa kwa program ya P4R III na Mkandarasi Utonde Construction & General Supplies na utanufaisha wakazi 7920 katika vijiji vya Byunga na Mwabuluda.
Ameongeza kuwa Mradi wa Maji Gusuma unatekelezwa kwa gharama ya shilingi mil. 426 kwa program ya P4R III na mkandarasi Utonde Construction & General Supplies na utahudumia wakazi 9910 wa vijiji vya Gasuma na Bulumbaka.
‘’Mradi wa Maji Ibulyu unatekelezwa kwa gharama ya shilingi Mil. 404 kwa program ya P4R III na mkandarasi Ursino Company Ltd kwa muda wa miezi saba, mradi huu utanufaisha wakazi 6580 wa kijiji cha Ibulyu’’ amesema.
Ameongeza kuwa watahakikisha wanasimamia utekelezaji wa miradi ya Maji kwa kuzingatia Ubora, Viwango na Mkataba ili thamani ya fedha kwenye miradi hiyo iweze kuonekana.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mwadobana Duka Mashauri ameipongeza serikali kuendelea kutekeleza miradi ya maji vijijini ambayo imewatua ndoo akina mama ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Lucia Kadikilo mkazi wa Kijiji cha Mwabuluda ameipongeza serikali kutekeleza miradi ya maji vijiji ambapo itawaondolea akina mama adha ya kufuata maji umbali mrefu.
Masunga Bija Mkazi wa Byuna amesema wameupokea mradi wa maji ili kuwaondolea adha ya maji, kwani huko nyuma akina mama walikuwa wanatoka nyakati za usiku kufuata maji mtoni ambayo hayakuwa safi na salama.
MWISHO.
إرسال تعليق