Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, akizungumza na watumsihi wa serikali Mkoa wa Simiyu (hawapo pichani) leo mjini Bariadi. |
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka watumishi na watendaji wote wa serikali kuhakikisha wanasimamia vyema miradi yote ya serikali inayotekelezwa katika maeneo yao ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaoendana na thamani iliyotumika.
Aidha Majaliwa amesisitiza kuwa suala la usimamizi wa miradi na thamani ya fedha ni muhimu sana lizingatiwe kwani kufanya hivyo kutasaidia kupeleka mradi kulingana na uhitaji wa eneo husika badala ya kupeleka mradi sehemu ambayo thamani yake haitaonekana.
Waziri Mkuu ameyabainisha mapema leo wakati akizungumza kwenye kikao cha watumishi wa umma kutoka idara mbalimbali za mkoa wa Simiyu kilichofanyika mjini Bariadi huku akielekeza pia kuwepo kwa usimamizi wa karibu wa miradi yote ya serikali.
"Watendaji wa kawaida, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Watendaji wengine simamieni miradi yenu ianze na kukamilika kwa wakati na ni muhimu sana thamani ya mradi na fedha iliyotumika viendane" Amesema Waziri Mkuu
Akizungumza katika kikao hicho Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya Dk. Festo Dugange amesema kuwa serikali inaendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma pamoja na kupeleka watumishi katika maeneo yenye upungufu.
Dk Dugange amesema kuwa serikali inatambua changamoto ya upungufu wa Watumishi katika Mkoa wa Simiyu lakini inashirikiana na Watumishi waliopo ili kuhakikisha kuwa dhamira ya serikali kuwahudumia wananchi na kuboresha huduma inatekelezwa.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 2 serikali imeleta watumishi wa kada ya afya 277 ambapo kwenye elimu ni 587 kwa lengo la kupunguza mzigo na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Awali akizungumza katika kikao hicho mkuu wa mkoa huo Dk. Yahaya Nawanda amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2022/2023 Mkoa umejiwekea malengo ya kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 10.7 na kwamba hadi kufikia februari umefanikiwa kukusanya bilioni 6.76 sawa na asilimia 63 ambapo kufikia mwezi mei utakuwa umefanikiwa kwa asilimia asilimia 100.
Mwisho.
Post a Comment