Na Mwandishi wetu Simiyu.
Maadhimisho ya siku ya kifua kikuu Dunia kitaifa
yanatarajiwa kufanyika Mkoani Simiyu Machi 24, 2023, ambapo Mgeni rasmi
anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim
Majaliwa.
Kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika katika
uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani humo, ambapo kauli mbiu kwenye
maazimisho hayo ni kwa pamoja tunaweza kutokomeza kifua kikuu nchini Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo Mjini
Bariadi, Mratibu wa kitaifa wa masuala ya Ulaghabishi, mawasiliano na
uhamasishaji kutoka Mpango wa kitaifa wa kifua kikuu na Ukoma Wizara ya Afya Jilius
Mtemahanji,
Amesema kuwa katika maadhimisho hayo, Waziri Mkuu
anatarajiwa kuzindua mkakati rasmi wa kisekta wa mapambano dhidi ya kifua kikuu,
ambao unalenga kuongeza mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Katika maazimisho hayo, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt.
Boniphace Marwa, amesema shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwemo wananchi
kuelimishwa jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo.
Dkt. Marwa amesema kuwa mkoa wa Simiyu kuwa
mwenyeji kitaifa ni fursa kubwa kwa wananchi wake kuweza kufungua ufahamu na
uelewa juu ya ugonjwa wa kifua kikuu.
“ Kwenye maadhimisho haya kutakuwepo na huduma
mbalimbali kama upimaji wa watu wenye ugonjwa huo, zoezi ambalo litafanywa na
gari maalumu lenye vifaa vya upimaji na watakaobainika wataanzishiwa dawa,”
amesema Dkt. Marwa.
Naye Mratibu wa kifua kikuu Mkoa wa Simiyu Emmanuel
John amesema kuwa Mkoa huo, ni miongoni mwa mikoa ambayo kumekuwepo na ongezeko
la wagonjwa wa kifua kikuu.
Mratibu huyo amesema kuwa ongezeko hilo linatokana
na kuwepo wa Shughuli za uchimbaji wa madini katika maeneo mbalimbali, lakini
pia kuboreshwa na huduma za upimaji wa wagonjwa wenye ugonjwa huo.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment