Wakazi 120,000 Mji wa Maswa Wakosa Huduma ya Maji, MAUWASA yatoa Sababu

Sehemu ya chujio la Maji katika chanzo Cha Maji Cha Bwawa la New Sola katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu likiwa halifanyi kazi Kwa sasa baada ya Tanesco kukata Umeme kwenye mtambo wa kusukuma Maji kwenye bwawa hilo.


Sehemu ya Bwawa la New Sola linalomilikiwa na Mauwasa likiwa na Maji ya kutosha kuweza kuwahudumia Wateja wake kwa zaidi ya Mwaka mmoja kutokana na mvua zinazoendelea kuonyesha katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Simiyu.


Na Samwel Mwanga, Maswa.
  

ZAIDI ya Wakazi 120,000 wa Mji Maswa na vijiji 11 katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu wanaopata huduma ya Maji safi na salama kupitia Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa (MAUWASA) wamekosa  huduma ya Maji.

 

Wakazi hao wanaikosa huduma ya Maji kufuatia Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuikatia umeme mitambo ya kusukuma maji ya Mauwasa iliyoko katika Kijiji Cha Zanzui.

 

Imedaiwa kuwa TANESCO wamechukua hatua hiyo kutokana na kuidai Mamlaka hiyo ya Maji kiasi cha Mil. 264 deni ambalo ni la muda mrefu.

 

Kufuatia hali hiyo, wakazi hao sasa ni siku tatu hawajapata huduma ya Maji safi na salama  na kuwalazimu kupata Maji kwenye visima na madimbwi ambayo si safi na salama

 

Wakizungumza na Wandishi wa habari mjini Maswa ambao walitembelea mji huo kujionea hali halisi baadhi ya wananchi hao ambao kwa sasa wanapata shida ya kupata huduma ya maji walisema kuwa hali hiyo inawalazimu
kutumia maji hayo ya  madimbwi na visima hivyo  vilivyoko kwenye mito ya maji inayozinguka mji huo.

 

Walisema kwa sasa hali imekuwa mbaya sana na wanatumia muda mwingi kutafuta maji ambayo nayo yanapatikana katika vyanzo hivyo huku
wakinunua dumu moja lenye ujazo wa lita 20 kwa gharama ya Shilingi 500 hadi Shilingi 800 na hata na wakati mwingine wanashindwa kuoga na kufanya shughuli zingine zinazo hitaji huduma hiyo.
 

 

“Hapa sisi tuna shida ya maji dumu moja la lita 20 tunanunua kwa gharama ya kuanzia Sh 500 hadi shilingi  800 tunashindwa kuoga na unaweza ukakaa kutwa maji hayapatikani…kutokana na uhitaji na maji tunanunua kwa
wafanyabiashara ambayo si safi na salama na afya zetu ziko hatarini kupata magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.” alisema Maria John.


Walisema wameshangazwa  kwa kitendo cha Tanesco kuwahukumu wao wakati  wamekuwa wakitimiza wajibu wao kwa kulipa ankra za Maji kila mwezi huku wakiwaomba Viongozi wa Wizara ya Nishati na Viongozi wa Wizara ya Maji kukutana na kutatua tatizo hilo.


 

“Sisi wateja wa Mauwasa  kila mwezi tumekuwa tukilipa bill zetu za maji hata ukichelewa kulipa kwa wakati wanakusitishia huduma ya maji hii adhabu sisi haituhusu ni vizuri Viongozi wa juu wa Wizara ya Nishati na wale wa Wizara ya Maji wakutane walipatie ufumbuzi suala hiliaana tunateseka sana,"alisema John Samson.


 

Walisema kuwa wao wateja walishatimiza wajibu wao wa kulipa akra zao za matumizi ya maji kwa Mamlaka hivyo wanapaswa kuendelea kupata
huduma hiyo na suala la kukatiwa umeme kwenye mitambo hiyo haliwahusu na hivyo kuwataka kutafuta njia mbadala ili waweze kuendelea
kupata huduma ya maji kulingana na mikataba waliyowekeana.

 

“Suala la umeme kwa Shirika la Tanesco kuwakatia Mauwasa kwa ujumla sisi halituhusu kabisa maana sisi tukiwa wateja tulishatimiza wajibu wetu wa kulipia ankra zetu za maji kwa kila mwezi hivyo tunapaswa kuendelea kupata
huduma ya maji" amesema na kuongeza.

 

" Hivyo ni vizuri sasa wakatafuta njia mbadala ya kupata umeme ili tuendelee kupata huduma ya maji safi ukizingatia mji wetu hauna vyanzo vya maji mbadala vya uhakika isipokuwa bwawa la New Sola ambalo ndilo linatuhudumia kupitia Mauwasa, kuna hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko ,”alisema Mwashi Manoni.

 

Akizungumzia Hali hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa MAUWASA, Mhandisi Nandi Mathias alikiri Kwa Tanesco kuwakatia umeme kwenye mitambo hiyo kutokana na kuwepo kwa deni hilo la siku za nyuma ambalo lilishawasilishwa Hazina Kwa ajili ya malipo.

 

Mhandisi Nandi alisema kuwa siku za nyuma Mamlaka hiyo ilikuwa ikilipiwa umeme na serikali kupitia Wizara ya Maji na deni hilo lilikuwa Shilingi Bilioni 1.9 lakini zimelipwa na kubaki Sh Milioni 264 na Hazina wanafahamu deni hilo maana wao ndiyo wanaotoa fedha,"

 

"Sisi kwa sasa tunajiendesha kwa kujilipia umeme kila mwezi kiasi cha Sh Milioni 30 kupitia makusanyo yetu ya ndani msingi huo deni hilo la siku za nyuma litalipwa na serikali kupitia Hazina na Mauwasa,"alisema.

 

Mhandisi Nandi alisema kuwa kwa sasa suala hilo linashughulikiwa na Uongozi wa Serikali ya wilaya ya Maswa pamoja na Serikali ya Mkoa wa Simiyu Ili kuhakikisha huduma ya Maji inarejea kwani ni muhimu kwa Wananchi.

 

"Hivyo basi, wateja wanashauriwa kuwa na subira wakati suala hili linafuatiliwa  kwa karibu na uongozi wa wilaya na mkoa ukishirkiana na uongozi wa Mamlaka ya Maji ili Umeme uweze kurejeshwa kwa haraka kadri itakavyowezekana kwa kutambua umuhimu mkubwa wa huduma hiyo kwa wananchi,"alisema.

 

Aidha Mhandisi Nandi ameomba radhi kwa usumbufu wowote unaojitokeza kwa wateja wake huku akisisitiza kuwa "Sisi kwa sasa tunajiendesha kwa kujilipia umeme kila mwezi kiasi cha Sh Milioni 30 kupitia makusanyo yetu ya ndani  Kwa msingi huo deni hilo la siku za nyuma litalipwa na serikali kupitia Hazina na si Mauwasa,".

 

Mamlaka hiyo chanzo chake kikuu cha Maji ni bwawa la New Sola na inahudumia zaidi ya watu  120,000 na mifugo ipatayo 50,000 katika mji wa Maswa na vijiji 11 ambavyo ni pamoja na Zanzui, Malita, Mwabayanda, Mwashegeshi, Hinduki, Mwadila, Buyubi, Mwasita, Ngwigwa, Iyogelo na Badabada.

 

MWISHO.

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post