Na Samwel Mwanga, Maswa.
MRADI wa BOOST unaolenga kuboresha Elimu ya Awali na Msingi umeleta faraja kwa Wanafunzi, Walimu na Wananchi katika wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu kwenye shule nane zenye msongamano wa wanafunzi na upungufu wa vyumba vya madarasa, madawati na matundu ya vyoo vyote hivyo vimepatiwa ufumbuzi.
Jumla ya Shilingi Bil. 1.5 zimetumika katika utekelezaji wa mradi huu katika wilaya ya Maswa ambapo tayari ujenzi umekamilika wa shule mpya tatu na vyumba vya madarasa 13 na matundu ya vyoo 14 .
Fedha hizo zimetolewa na Serikali pamoja na Benki ya Dunia na utekelezaji wa Mradi huu hapa nchini ni kwa miaka mitano kuanzia mwaka huu hadi mwaka 2025/2026 na kuzinufaisha halmashauri zote 184 hapa nchini ikiwemo na halmashauri ya wilaya ya Maswa.
Wakizungumza na Waandishi wa habari kwa nyakati na maeneo tofauti tofauti waliotembelea shule nane zinazotekeleza mradi huo wilayani humo ili kujionea uboreshaji wa miundo mbinu ya elimu kwa madarasa ya awali na msingi Wanafunzi, Walimu na Wananchi wameipongeza serikali kwa kutekeleza mradi huo ambao umewaletea faraja kubwa sana.
Wamesema kuwa shule hizo zimekuwa na msongamano mkubwa wa wanafunzi hata kuwafanya walimu washindwe kuwahudumia wanafunzi wao mmoja mmoja kwani kawaida darasa moja linapaswa kuwa na wanafunzi 40 lakini kwa sasa darasa moja limekuwa na wanafunzi zaidi ya 100.
“Shule ya Msingi Ipililo B’’ ina jumla ya wanafunzi 1429 na vyumba 9 tu vya madarasa hivyo kuwafanya wanafunzi zaidi ya 100 kusomea katika darasa moja na kwa hali hii huwezi kumsaidia mwanafunzi mmoja mmoja kutokana na wingi huo hivyo kujengwa kwa madarasa matatu ya kisasa kwenye shule yetu hii kupitia Mradi wa BOOST kwetu ni faraja itatupunguzia mrundikano huu wa wanafunzi kwenye darasa moja,” amesema Mwl. Pili Sanane ambaye ni Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Ipililo B.
Wameendelea kueleza kuwa kufuatia kutolewa kwa elimu bila malipo kwa wanafunzi wa shule ya awali hadi kidato cha sita kumefanya ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi katika shule hasa za Msingi na hiyo yote inatokana na mwamko wa wananchi kuwapeleka watoto wao shule huku serikali ikilia msisitizo jambo hilo.
“Baada ya serikali kutoa elimu bila malipo kuanzia shule za Msingi hadi kidato cha sita kumekuwa na wimbi kubwa la uandikishaji hasa wa wanafunzi wa darasa la awali na darasa la kwanza kwa shule za msingi hali hiyo imeendelea kwa kasi ndiyo maana leo kwenye shule yetu ya Jija A tuliletewa fedha na tumejenga shule nyingine mpya yenye mikondo miwili miwili hii kwetu sisi ni faraja kubwa sana maana wanafunzi wengine watahamia kwenye hii shule mpya,”amesema Mathayo Bujenja ambaye ni Mwalimu Mkuu shule ya Msingi Jija A.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nguliguli, Mwl Rameshi amesema kuwa licha ya shule yake kujengewa madarasa mawili pamoja vyoo vimesaidia kupunguza mlundikano wa muda mrefu hasa nyakati za mapumziko wanafunzi wamekuwa wakitumia muda mrefu kujisaidia.
“Katika vyoo tulikuwa na mrundikano mkubwa wa wanafunzi hasa wakati wa mapumziko walikuwa wakijipanga foleni ili kuingia chooni kujisaidia na hivyo walikuwa wanatumia muda mwingi sana sisi muda wetu wa mapumziko ni dakika 20 tu lakini kutokana na hali hiyo inabidi tutumie muda zaidi ya huo uliowekwa na serikali ila kwa sasa hali hiyo imepungua baada ya vyoo kukamilika,”amesema.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ambazo mradi huo unatekelezwa walisema kuwa kwa sasa wamepata faraja kubwa kutokana na kusoma katika mazingira rafiki ambayo kwa sasa mrundikano katika darasa moja umepungua sambamba na kusoma wakiwa wamekaa kwenye madawati.
“Darasani tulikuwa tunasoma tuko wanafunzi wengi katika darasa moja na pia tulikuwa wengine tunakaa chini ya sakafu lakini kwa sasa tuko kwenye darasa jipya tunasoma vizuri na tunakalia madawati hivyo hata kujifunza kwetu kumekuwa ni kuzuri sana,”amesema Msabi Yoha ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Mwakabeya.
Naye Charles Malinzuri ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Igunya amesema kuwa katika utekelezaji wa mradi huo katika shule yao hakuna hata mwananchi mmoja aliyechangishwa kiasi cha fedha tofauti ilivyokuwa siku za nyuma wakikimbizana na wananchi katika michango ya ujenzi wa shule hivyo ameishurukuru sana serikali kwa kutekeleza mradi wa BOOST.
“Sisi hapa Igunya kwa kweli tunamshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutuletea mradi huu wa BOOST maana hakuna hata mwananchi mmoja ambaye amechangishwa kiasi chochote cha fedha na tumejengewa madarasa ya kisasa hakuna ile hali ya kukimbizana na wananchi kwa ajili ya michango kama ilivyokuwa huko kwa siku za nyuma,”amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu kwa kuipatia halmashauri hiyo kiasi cha Sh Bilioni 1.5 katika sekta ya elimu kwa ajili ya kuboresha miundo mbinu ya elimu ya Awali na Msingi kupitia mradi wa BOOST.
Amesema kuwa wilaya hiyo yenye majimbo mawili ya Uchaguzi ya Maswa Mashariki na Maswa Magharibi wameweza kutekeleza Mradi huo na kuyagusa majimbo yote kulingana na uhitaji kwa kila eneo.
''Katika wilaya
ya Maswa mradi wa BOOST kwa jimbo la Maswa Magharibi umetekelezwa kwa kujenga
Vyumba vya madarasa Viwili na Matundu matatu ya vyoo katika shule ya msingi
Igunya kwa gharama ya Shilingi Mil. 56.3.'' amesema Mtipa
amefafanua kuwa, Shule mpya ya Msingi yenye mikondo Miwili katika kijiji cha Jija kwa gharama ya Shilingi Mil. 540.3, Vyumba viwili vya madarasa na darasa la Awali la mfano kwa gharama ya Shilingi Mil. 69, katika shule ya msingi Mwabayanda na Shule mpya ya msingi yenye mkondo mmoja mmoja katika kijiji cha Shishiyu kwa gharama ya Shilingi Mil. 348.5.
''Kwa upande wa
Jimbo la Maswa Mashariki, Mtipa amesema wameweza kutekeleza mradi wa BOOST kwa kujenga Vyumba
Vitatu vya Madarasa na matundu matatu ya vyoo katika shule ya msingi Ipililo B''
kwa gharama ya Shilingi Mil. 81.3.'' amesema na kuongeza.
''Shule mpya ya msingi yenye mkondo mmoja katika kijiji cha Mwakabeya kwa gharama ya Shilingi Mil. 348.5, Vyumba Vitatu vya madarasa na matundu matatu ya vyoo katika shule ya msingi Ngudu kwa gharama ya Shilingi Mil. 81.3 na Vyumba Viwili vya madarasa na matundu matatu ya vyoo katika shule ya msingi Nguliguli kwa gharama ya Shilingi Mil. 56.3.''
Aidha amesema kukamilika kwa mradi huo katika maeneo hayo kwenye halmashauri hiyo kutapunguza mrundikano wa wanafunzi kwenye shule hizo ambazo pia vyumba vya madarasa vimewekewa madawati sambamba na kuboresha mazingira ya kufundishia kwa walimu hasa kwenye madarasa ya Awali.
MWISHO.
Mwl Mkuu wa Shule ya Msingi Jija A, wilayani Maswa Mkoani Simiyu Mathayo Bujenja akitoa maelezo mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya utekelezaji wa Mradi wa BOOST.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
إرسال تعليق