Wakulima wa mbogamboga katika Kijiji cha Mwabayanda (M) katika Kata ya Ngh'wigwa wilayani Maswa Mkoani Simiyu wakipata mafunzo ya kilimo Cha Mbogamboga.
Samwel Mwanga, Maswa.
WAKULIMA 100 wa Mazao ya Mbogamboga kutoka katika Kata tano za Halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wamepatiwa mafunzo ya uzalishaji wa mazao hayo ili kuweza kuongeza tija katika uzalishaji.
Pia wakulima hao kutoka Kata za Nyalikungu, Binza, Ng’hwigwa, Zanzui na Malita wamepatiwa mafunzo ya umuhimu wa mbogamboga katika kuboresha lishe kwa jamii.
Akifungua mafunzo hayo mjini Maswa, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika Halmashauri hiyo, Robert Urassa amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wakulima hao ambao ni Wanawake na Vijana ili waweze kuzalisha kwa tija katika mazao yao ya bustani hasa mbogamboga.
Amesema kuwa kilimo cha mazao ya bustani kinapendwa na vijana kutokana na kutoa matokeo kwa haraka na hivyo kujipatia kipato kwa muda mfupi kutokana na mazao hayo kukomaa kwa muda mfupi.
“Hiki kilimo cha mazao bustani kimekuwa kinapendwa sana na Vijana kutokana na kuwa kinatoa matokeo ya haraka na ukizingatia vijana wanataka kipato cha haraka na ukizingatia haya mazao ni ya muda mfupi,”amesema.
Amesema kuwa kilimo cha bustani kinahitaji usimamizi wa karibu hivyo ni vizuri wakulima wanaojihusisha nacho hasa wale wa mazao ya mbogamboga wajiunge kwenye vikundi ili waweze kupatiwa mikopo kwa ajili ya kupata pembejeo kama ilivyo kwa wakulima wa mazao mengine kama vile pamba.
Akizungumzia umuhimu wa mboga za majani kwa afya ya binadamu kwa jamii amesema kuwa ni vizuri jamii iweze kulima mazao ya bustani ili kuweza kuzipata mboga hizo ambazo pia husaidia kuinua kipato kwa familia
Ameongeza kuwa wakulima hao wamepewa mafunzo ili wakawafundishe wakulima wengine waliopo katika Kata zao ili waweze kuzalisha mazao hayo ya bustani hasa ya mbogamboga ili kuongeza kipato kwa wakulima ikiwa ni kusaidia juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa wakulima wananufaika na kilimo chao.
“Mafunzo haya ni muhimu sana kwenu wakulima wa bustani hasa wa mbogamboga na ninyi mtakuwa chachu katika maeneo yenu kwenda kuwafundisha wakulima wenzenu ili waeze kuzalisha kwa tija sambamba na kutunza mazao kwa kupuliza viuatilifu ambavyo havitakuwa na madhara kwa binadamu ambao watayatumia kama lishe,”amesema.
Naye Mtaalamu wa Mbogamboga na Matunda kutoka Halmashauri ya wilaya hiyo, Masalu Lusana amesema kuwa ni vizuri wakulima hao wakatumia mbolea na viuatilifu kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa kilimo ili kuweza kupata tija kwenye mazao yao.
Naye Barnabas Richard ambaye ni mkulima kutoka Kata ya Nyalikungu amesema kuwa mafunzo hayo yatamsaidia sana kwa kuwa alikuwa akilima tu kilimo cha mazoea ambacho kilikuwa kinampa mavuno kidogo na sasa anakwenda kufanya mabadiliko ya kilimo ambacho anaamini kitampatia mazao mengi.
Amesema kuwa watakuwa mabalozi wazuri kwa wakulima wengine kwa kutumia mafunzo waliyo yapata na kuisaidia jamii kwa kuwa walikuwa wakihitaji mafunzo hayo kwa muda mrefu na wanaishukuru serikali kwa kuwakumbuka.
MWISHO.
Mtaalamu
wa mbogamboga na matunda kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Maswa,Masalu Lusana
akitoa mafunzo kwa Wakulima wa mbogamboga juu ya kilimo chenye tija.
إرسال تعليق