Na Samwel Mwanga,Bariadi
KATIBU wa Siasa, Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Amos Makala,amedai kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiko katika mwelekeo wa kupotea kisiasa baada ya uchaguzi mkuu wa 2025 kwa kuwa,hakitakuwa hata diwani wala mbunge.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Alhamis,Mei 22,2025 katika mji wa Bariadi amesema kuwa kutoshiriki kwa chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao pamoja na msimamo wake wa "No Reform, No Election" kumeathiri ushawishi wake kwa wanachama wake waliotaka kugombea nafasi hizo na kukidhoofisha chama hicho.
"Chadema hawatakuwa na mtu hata mmoja, si diwani, si mbunge,kwa hiyo ruzuku hawatapata,mara baada ya uchaguzi wa mwaka huu 2025 kuelekea mwaka 2030, chama hicho kitakuwa historia hakitakuwepo," amesema.
Kauli hiyo inakuja wakati taifa likijiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba mwaka huu, huku baadhi ya vyama vya upinzani vikiendelea kukosoa mfumo wa uchaguzi na kutaka mabadiliko zaidi, licha ya kuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi chini ya marekebisho ya kisheria yaliyofanywa na serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa kwa mantiki hiyo, hakuna sababu ya kuahirisha au kusogeza mbele uchaguzi huu, hasa kwa kuwa nchi ipo katika hali ya amani.
“Kauli ya kutoshiriki uchaguzi haina mashiko, na wananchi waelewe kuwa uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa,”
“Kauli ya "No reform, no election" haina msingi wa kikatiba,uchaguzi si suala la hiari bali ni takwa la kikatiba,huu si uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bali wa taifa, vyama vya siasa vina wajibu wa kushiriki ili kutoa fursa kwa wananchi kuchagua viongozi wao,”amesema.
Amesema licha ya chadema kupita maeneo mbalimbali ya nchi na kufanya mikutano na kueleza kuwa hakuna mabadiliko yaliyofanyika katika sheria na kanuni za uchaguzi lakini niwaeleze wananchi mabadiliko yamefanyika.
“Mabadiliko makubwa yamefanyika chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. maoni ya vyama vya siasa, ikiwa ni pamoja na Chadema, yalizingatiwa na tukapata sheria mpya mbili muhimu,”
“Sheria hizo ni pamoja na kuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo uteuzi wa wajumbe wake sasa unafanyika kwa uwazi pamoja na kuanzishwa kwa sheria mpya ya uchaguzi wa wabunge na madiwani, inayoruhusu usimamizi wa uchaguzi kufanywa na viongozi waandamizi wa umma na kuhakikisha wagombea wanapita bila pingamizi zisizo na msingi,”amesema.
Makala amesema kuwa ruzuku ya zaidi ya Sh110 milioni inayopokelewa na Chadema kila mwezi haiwezi kuendelezwa kama chama hicho hakitashiriki uchaguzi wala kupata wawakilishi wa kuchaguliwa.
"Wameamua kujiondoa kwenye mchakato wa uchaguzi, hivyo hata hii ruzuku waliyokuwa wanaipata hawataipaya tena maana hawatakuwa na wawakilishi wowote bungeni na kwenye mabaraza ya madiwani kwani wameamua kujipumzisha wenyewe,”amesema.
Kwa upande mwingine, Makala amesema kuwa anapenda kuwapongeza viongozi wa Chadema ambao ni Tundu Lissu na John Heche kwa kuwa na ujasiri wa kutoa kauli kali za kisiasa kwani waliahidi "kukinukisha" na kweli wamekinukisha, lakini matokeo yake yameonekana kuwa kinyume kwa kudhoofisha chama chao kwa mikono yao wenyewe.
‘Kwa hiyo, kwa wananchi wa Simiyu na Tanzania kwa ujumla, tunathibitisha kuwa mabadiliko yamefanyika, mazingira yameboreshwa na uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa,” amesema.
Makala anafanya ziara ya kikazi ya siku mbili katika mkoa wa Simiyu na atamalizia ziara yake katika wilaya ya Maswa kwa kuhutubia mikutano miwili mjini Maswa na Njiapanda ya Malampaka kabla ya kuhitimisha ziara yake katika mkoa huo.
MWISHO.
إرسال تعليق