
Na Samwel Mwanga,Maswa.
MAMLAKA ya Mji Mdogo wa Maswa mkoa wa Simiyu imeitaka halmashauri ya wilaya hiyo kuiruhusu kukusanya mapato yake moja kwa moja kwa kupewa vyanzo rasmi vya mapato, ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuharakisha maendeleo ya mji huo.
Hayo yamesemwa Mei 8,2025 na Mwenyekiti wa mamlaka hiyo,Caroline Shayo wakati akizungumza katika kikao cha dharula kilichowakutanisha wajumbe wa mamlaka ya mji mdogo wa Maswa na viongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo.
Amesema kuwa kwa sasa wanashindwa kutekeleza majukumu mbalimbali likiwemo suala la usafi katika mji wa Maswa kutokana na ukosefu wa fedha na hivyo kuwepo kwa malundo ya taka jambo ambalo linatia kero na kuonekana uongozi wa mamlaka hiyo kutowajibika.
Amesema kuwa kwa sasa mamlaka hiyo haina uwezo wa kifedha wa kujitegemea kwa kuwa haina vyanzo vya mapato ilivyoidhinishwa rasmi kuvikusanya kwani mapato yote hukusanywa na halmashauri ya wilaya ya Maswa.
“Tuna uhitaji mkubwa wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali ya maendeleo katika eneo letu la mamlaka yetu lakini changamoto kubwa ni kwamba hatuna mamlaka ya kukusanya mapato kutoka kwenye vyanzo vilivyopo,tunaomba halmashauri ya wilaya itupatie mamlaka hiyo ili tuweze kuwahudumia wananchi ipasavyo,” amesema.
Alitaja baadhi ya maeneo ambayo mamlaka hiyo ingeweza kukusanya mapato kuwa ni mnada wa Shanwa,masoko, stendi ya mabasi, maegesho ya magari, na vibanda vya biashara, lakini vyanzo hivyo kwa sasa vinasimamiwa na halmashauri ya wilaya.
Tatu Ally ni mwenyekiti wa kitongoji cha Sola amesema kuwa kabala ya mamlaka hiyo kuanza kukusanya mapato ni vizuri wajumbe wote wa baraza la Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa ikafanya ziara ya kuvitembelea vyanzo hivyo vya mapato ili waweze kuvifahamu.
“Kabla ya kukabidhiwa hivi vyanzo vyetu vya mapato ni vizuri tufanywe ziara ya kuvitambua na hii itatusaidia kuhakikisha hakuna mapato yatakayovuja na lengo letu ni kuhakikisha tunawahudumia wananchi waliotuweka madarakani,” amesema.
Naye Abudlasack Msuya ambaye ni Mwenyekiti wa kitongoji cha stendi mpya amesema kuwa mapato yanayotokana na ukusanyaji wa ushuru katika kituo kikuu cha mabasi mjini Maswa ni makubwa iwapo yatasimamiwa kikamilifu na hicho ni miongoni mwa chanzo muhimu katika mamlaka hiyo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa,Maisha Mtipa amesema kuwa kwa utaratibu wa sasa halmashauri hiyo ndiyo iliyokuwa ikikusanya mapato katika eneo la mamlaka hiyo na kurejesha asilimia 40 ya mapato.
“Mji mdogo sasa mjipange ili muweze kusimamia na kukusanya mapato yenu katika eneo lenu,na sasa niagize Mtendaji wa Mamlaka uteue watu kutoka mamlaka yako uwaingize kwenye ile timu ya kukusanya mapato ya halmashauri ili nao wajifunze kukusanya mapato,mie ndiye msimamizi wa mapato ni lazima niwe makini ili mapato yasiweze kupotea,”.
“Ninaamini mamlaka mkikusanya mapato kutasaidia sana katika kuharakisha huduma kwa jamii, hasa kwenye usafi wa mazingira,” amesema.
Slivester Lugembe ni mkazi wa mji wa Maswa anasema kuwa kwa sasa baadhi ya huduma ndani ya mji huo hazitekelezeki kwa wakati kwa sababu mamlaka hiyo inasubiri fedha kutoka halmashauri mama, jambo linaloathiri utekelezaji wa haraka wa miradi ya maendeleo.
“Kuna wakati takataka zinakusanywa katika maeneo mbalimbali zinahitajika kutolewa na kusafishwa haraka kupelekwa kwenye dampo la taka lakini fedha hazipo,ikiwa mamlaka ya mji mdogo itapewa uwezo wa kukusanya mapato, mambo kama haya yatafanyika kwa wakati,” amesema.
Esther Pachal ni mkazi wa mtaa wa Sokoni mjini Maswa anasema kuwa huduma za usafi na ukusanyaji wa taka zimekuwa zikitolewa kwa kusuasua, hali inayosababisha uchafu kujaa katikati ya mji.
“Tungependa kuona mamlaka ya mji mdogo inakuwa na uwezo wa kifedha ili iweze kuajiri watu wa usafi, kuweka vibao vya biashara, na hata kujenga vyoo vya umma,” amesema.
Maswa ni miongoni mwa miji midogo inayokua kwa kasi katika mkoa wa Simiyu, lakini changamoto ya rasilimali fedha imekuwa kikwazo kikubwa kwa utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya haraka kwa wakazi wake.
MWISHO
Post a Comment