RC Mara aagiza wananchi wa Nyatwali kuhama baada ya kulipwa fidia .

 

Ronard Mochomba (mwenye kipaza sauti) kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti akitoa maelezo kwa Mkuu wa mkoa wa Mara,Kanali Evance Mtambi(kulia) jinsi alivyotengeneza mfano wa mnyama nyati kwa kutumia vyuma chakavu.


Na,Samwel Mwanga,Serengeti



MKUU  wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi, amewaagiza wananchi wa Kata ya Nyatwali, Wilaya ya Bunda, kuhama mara moja katika maeneo waliyoishi baada ya kulipwa fidia na serikali ili kupisha eneo la ushoroba wa wanyama pori wanaopita kuelekea Ziwa Victoria kutafuta maji.



Amesema hayo Mei 5,2025 mjini Mugumu wilaya ya Serengeti mkoani Mara wakati akizungumza katika maadhimisho ya kilele cha siku ya urithi wa dunia,Afrika yaliyofanyika  kwenye uwanja wa michezo wa Sokoine.



Amesema kuwa serikali imeshatoa kiasi cha Sh 53 bilioni kama fidia kwa wakazi wa kijiji hicho ili kuanzisha rasmi ushoroba huo unaopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. 



Amesisitiza kuwa eneo hilo limeshatangazwa rasmi kuwa hifadhi kupitia Tangazo la Serikali (GN) Na. 269 ya  mwaka 1974 na hivyo haliruhusiwi kuwa na makazi ya watu.



"Serikali imelipa fidia kwa wananchi,wale wananchi wa  Nyatwali ambao tayari wamekwisha lipwa fidia ni muhimu waanze taratibu za kuondoka ili kupisha ushoroba wa wanyama na kupunguza migogoro ya binadamu na wanyamapori, hasa tembo wanaokwenda Ziwa Victoria kutafuta maji," amesema.



Amesema wananchi wamekuwa wakiishi maisha ya wasiwasi kutokana na uvamizi wa mara kwa mara wa wanyama pori katika makazi yao, hali inayohatarisha usalama wao na wa mali zao.



"Katika maadhimisho ya siku ya leo kauli mbiu yake inasema kwamba majanga na migogoro ni tishio kwa urithi wa dunia hivyo ili kuepusha migogoro katika ya wanyama na binadamu ndiyo maana serikali imeamua kutoa fidia kwa wananchi hao ili kupiaha eneo hilo,"amesema.



Pia amesema kuwa maeneo yote ya urithi wa dunia yako 147 na kati ya hayo saba yako hapa nchini  ambayo ni hifadhi za Taifa,Misitu,Utamaduni,Lugha za Asili na maeneo ya kihistoria hivyo ni vizuri kuyatunza maeneo hayo kwa kufuata sheria zilizowekwa.



Aidha, amewataka wananchi hao kutosikiliza watu wanaopotosha au wanaotafuta umaarufu wa kisiasa kwa kueneza taarifa zisizo sahihi kuhusu zoezi hilo la fidia na uhamishaji.



Kwa mujibu RC Mtambi, amesema kuwa serikali inaendelea kulipa fidia kwa awamu kwa wananchi wa Kata hiyo ili kuhakikisha kila mkazi anapata haki yake kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa.



Mkurugenzi wa idara ya Malikale,Wizara ya Maliasili na Utalii,Zuberi Mabiye amesema kuwa vituo vya urithi ni lazima vitunzwe na kuendelezwa huku akisisitiza kuwa Hufadhi ya Taifa ya Serengeti ni moja ya tunu ya urithi wa Afrika.



"Kutangazwa kwa hifadhi ya taifa ya Serengeti  kuwa moja ya urithi wa  dunia ni fahari yetu watanzania hivyo niwaombe wananchi mnaoishi kando kando ya hifadhi hii tuilinde na kuitunza kwa vizazi vijavyo,"amesema.



Mkuu wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Stephano Msumi amesema kuwa wananchi wameilinda hifadhi hiyo na kuwa kivutio kikubwa cha urithi wa dunia hivyo wataendelea kushirikiana na jamii yote inayoizunguka hifadhi hiyo kwa ajili ya vizazi vijavyo.



"Tunahitaji kivutio hiki kuwa endelevu katika urithi wa dunia na hii yote inatokana na jinsi wananchi ulivyoshiriki kuilinda na sisi tunahaidi kuendelea kushirikiana nanyi ili kusudi hifadhi hii iweze  kunufaisha na vizazi vijavyo,"amesema.



Ana Kalumuna ni mwakilishi kutoka tume ya Taifa ya Unesco amesema kuwa wataendelea kujihusisha na usimamizi na ulinzi wa urithi wa dunia kwa vivutio vyote vilivyoko hapa nchini kwa kutoa ushauri wa kitaalam.



"Sisi Unesco tutaendelea kutoa ushauri wa kitaalam,kutunza maeneo yote ya kitamaduni,kutafuta raslimali,na kutunza urithi wa dunia kwa vivutio vyote vilivyopo hapa nchini,"amesema.



MWISHO.


Wanafunzi walioshiriki maandamano siku ya maadhimisho ya urithi wa dunia,Afrika.








Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post