
Na Samwel Mwanga, Simiyu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali imejipanga kuimarisha kilimo cha pamba kwa kuhakikisha zao hilo linapandishwa hadhi na kupewa thamani kama ilivyo kwa korosho na kahawa ambayo mazao makuu ya kimkakati nchini.
Dkt. Samia alitoa kauli hiyo leo, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Simiyu, ambapo ametembelea Wilaya ya Bariadi na kufungua viwanda viwili muhimu vya kuongeza thamani ya mazao,kiwanda cha kuchambua pamba na kiwanda cha kutengeneza mabomba ya maji vinavyomilikiwa na Kampuni ya MoliOil Milles Ltd.
Akizungumza na mamia ya ya wananchi waliojitokeza kushuhudia uzinduzi huo leo Jumatatu,Mei 16,2025, wa viwanda hivyo, Rais Samia alieleza kuridhishwa kwake na jitihada za wawekezaji wa ndani mkoani Simiyu walioamua kuwekeza katika viwanda vya kuchakata rasilimali za ndani.
"Nimefurahishwa sana na kuona wazawa wanawekeza kwa nguvu kubwa. Hili ni jambo la kujivunia kwa sababu linatoa ajira na kukuza uchumi wa mikoa yetu," amesema Rais Samia.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, alisisitiza kuwa uwekezaji huo utatoa ajira kwa vijana na kusaidia mnyororo wa thamani wa zao la pamba.
"Viwanda hivi vitakuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Simiyu na Taifa kwa ujumla. Ajira, mapato ya halmashauri na fursa kwa wakulima zitaongezeka," amesema Kigahe.
Mmoja wa wawekezaji, Emmanuel Gungu, alieleza kuwa mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita ndiyo yamewapa moyo wa kuwekeza.
"Tunamshukuru Rais Samia kwa kutufungulia milango. Sasa tunaweza kuchakata pamba hapa hapa Simiyu badala ya kuipeleka mbali," amesema Gungu.
Naye Njalu Silanga, muwekezaji mwingine, naye aliongeza kuwa uwekezaji huu utasaidia kuinua kipato cha wananchi wa kawaida na kuongeza mzunguko wa fedha katika jamii.
Milembe Silanga, akisoma risala kwa niaba ya wawekezaji, alimpongeza Rais kwa kutimiza ahadi ya kuleta viwanda kwa vitendo, tofauti na ahadi za maneno tu.
Katika hatua nyingine, Rais Samia alizindua jengo jipya la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, jengo la Halmashauri ya Mji wa Bariadi, shule mpya ya Wasichana ya Simiyu, pamoja na jengo la Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo.
MWISHO

إرسال تعليق