SERIKALI YAAGIZA UKAGUZI MFUMO WA TEHAMA HOSPITALI YA RUFAA SIMIYU.

 

Waziri wa Afya, Jenister Mhagama ( katikati) akizungumza na watumishi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Simiyu.


Na Samwel Mwanga,Simiyu.


SERIKALI imeagiza kufanyika kwa ukaguzi maalum wa mfumo wa TEHAMA katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Simiyu kufuatia wasiwasi wa uwepo wa dosari katika utendaji wa mfumo huo ambao unatajwa kuwa msingi wa utoaji wa huduma bora za afya nchini.


Agizo hilo limetolewa leo Jumapili, Mei 15, 2025 mjini Bariadi na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama baada ya kufanya ziara ya kukagua miundombinu na kuzungumza na watumishi wa hospitali hiyo.


Amesema kuwa pamoja na hospitali hiyo kuwa na mifumo ya kisasa ya TEHAMA, bado kuna changamoto zinazohusiana na ufanisi wa matumizi ya mifumo hiyo, ikiwa ni pamoja na taarifa za kupotea kwa baadhi ya vifaa na bidhaa za hospitali licha ya kuwepo kwa mfumo wa kidijitali unaopaswa kufuatilia kila hatua ya shughuli za kitabibu na utawala.


“Hospitali hii imewekwa mifumo ya kitehama, kama mfumo wetu umeunganishwa kwenye idara zote, inakuwaje tushindwe kudhibiti mwenendo wa shughuli zote, hili linatia mashaka,” alihoji.


Kwa mujibu wa Waziri, taarifa alizozipokea zinaonesha kuwa bado uongozi wa hospitali unategemea walinzi kufuatilia mali na vifaa, badala ya mifumo ya TEHAMA ambayo ingeweza kutoa taarifa kwa wakati halisi kuhusu uhamaji wa vifaa na dawa.


Amesema kuwa hali hiyo inaashiria uwezekano wa baadhi ya watumishi kuchezea mfumo huo ama mfumo wenyewe kutojiendesha kwa weledi.


Kutokana na hali hiyo,Waziri Mhagama amemuagiza, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalage,kupeleka timu maalum ya TEHAMA kutoka makao makuu ya wizara hiyo ili kufanya tathmini ya mfumo mzima na kubaini mapungufu.


“Mwambieni Katibu Mkuu alete timu ya TEHAMA kutoka wizarani, waje waangalie kama mfumo unafanya kazi zile tulizopanga kama serikali,hatutavumilia upotevu unaotokana na uzembe wa kiteknolojia,” amesema.


Naye,Mganga mkuu wa mkoa huo, Dk Boniphace Marwa, akiwasilisha taarifa ya hali ya afya mkoani humo, alishukuru serikali kwa uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya afya,hata hivyo,aliomba Wizara kuongeza idadi ya madaktari bingwa kwani hospitali hiyo bado inakabiliwa na uhaba mkubwa wa wataalamu hao.


“Huduma nyingi za kibingwa bado hazitolewi kwa kiwango kinachostahili kwa sababu ya uhaba wa madaktari bingwa,” amesema.


Mary John ni mkazi wa mji wa Bariadi amesema kuwa ziara ya waziri Mhagama imeibua maswali mapya kuhusu namna teknolojia ya Tehama inavyotekelezwa katika sekta ya afya.


“Kwa hili lililotokea katika hospitali yetu ya rufaa ya mkoa ni vizuri ukaguzi wa mifumo ifanyike katika hospitali zingine nchini ili kuhakikisha uwekezaji wa serikali unaleta matokeo tarajiwa kwa wananchi,”amesema.


Mariam Magesa ambaye ni mkazi wa wilaya ya Itilima amesema kuwa kauli ya waziri ni ya msingi kabisa kwani serikali imewekeza mabilioni kwenye mifumo ya TEHAMA, lakini bado huduma ni za kusuasua hivyo kama mifumo hiyo haifanyi kazi, basi kuna walioshindwa kazi.


"Suala la mfumo kutofanya kazi linaweza kuwa matokeo ya kutoweka wataalamu wenye ujuzi au kutokufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara,ufuatiliaji wa kitaalamu ni hatua nzuri, lakini isiishie Simiyu tu,"


"Hili ni onyo la wazi kuwa kuna uwajibikaji hafifu kwenye hospitali za umma. Kama mifumo ipo na bado vifaa vinapotea, basi kuna upotevu wa mali za umma unaopaswa kuchunguzwa kisheria."amesema.


MWISHO. 

Baadhi ya watumishi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Simiyu wakiwa kwenye kikao cha Waziri wa Afya, Jenister Mhagama (hayupo pichani).


Waziri wa Afya Jenister Mhagama (wa pili kushoto) akizungumza na viongozi wa hospitali ya mkoa wa Simiyu baada ya kukagua miundombinu ya hospitali hiyo.







Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم