![]() |
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
SERIKALI ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imetekeleza Miradi ya Maendeleo yenye thamani ya shilingi Bil.12.1 kwa muda wa miaka mitano kwenye Sekta za Afya, Elimu, Maji, Umeme, Barabara pamoja na mawasiliano katika kata ya Dutwa wilayani Bariadi Mkoani Simiyu.
Akizungumza kwenye mkutano maalumu wakati wa kuwasilisha Utekelezaji wa Ilani ya CCM (2020/2025), Mbunge wa Jimbo la Bariadi, Mhandisi Kundo Mathew amesema serikali ya Rais Dk. Samia imetekeleza Ilani ya CCM kwa kiwango kikubwa na kufungua fursa za uchumi, usafiri na usafirishaji.
Amesema, katika kata ya Dutwa kuna ongezeko la fedha za miradi ya maendeleo katika serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na kwamba wananchi wameona Utekelezaji wake katika maeneo yao.
"Ikifika mwezi Oktoba, tukampe kura za kutosha Rais Dk. Samia, tunamhemshimisha mama kwa kuwaambia wananchi juu ya fedha na miradi iliyotekelezwa...Kuna miradi ya Elimu, Afya, Maji, Umeme, Mawasiliano na Barabara" amesema Mhandisi Kundo.
Katika hatua nyingine, Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji ameipongeza serikali kwa kutekeleza Mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ambao Unatekelezwa kwa gharama ya shilingi Bil. 440.
Ameongeza kuwa ndani ua miaka mitano (2020/2025) kata ya Dutwa imepokea kiasi cha shilingi Bil.12 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, wakati huko nyuma (2015/2020), kata hiyo ilipokea kiasi cha shilingi Bil.3 kutekeleza miradi ya maendeleo kwa miaka mitano.
Awali, Diwani wa Kata ya Dutwa, Mkingwa Mapolu alimpongeza Mbunge wa Jimbo hilo aliyepigania na kuhakikisha Jimbo la Bariadi linakatwa ili kusogeza huduma wananchi.
Mapolu ameipongeza serikali kwa kutoa fedha ili kujenga miradi ya maendeleo pamoja na kuweka taa za Barabarani katika mji wa Dutwa.
Mwisho.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
إرسال تعليق