Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
CHAMA Cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA), kimesema Rais Samia Suluhu Hassan amebadilisha mifumo ya Utawala kwa kuruhusu mikutano ya kisiasa tofauti na awamu ya tano ambapo mikutano ya kisiasa ilikuwa imezuiwa.
Aidha kimesema Utashi wa kiongozi Mkuu wa nchi unaweza kulibadilisha taifa zima na kuondoa maumivu kwa wananchi ambao walikuwa wanahitaji kuonana na viongozi wa vyama vyao vya siasa.
Hayo yamesema jana na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe wakati akizungumza na wakazi wa Bariadi kwenye ufunguzi wa Mikutano ya chama hicho yaliyofanyika katika viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Mbowe amesema wanampongezea Rais Samia kwa kufanya jambo jema la kuruhusu mikutano ya kisiasa, kwa kutambua kuwa wanaliumza taifa hivyo akaamuru utawala wake usiendelee kuliumiza taifa.
‘’Nchi imebadilika, imekuwa shwari kama ni mikutano fanyeni, watu tunaonana leo, tunazungumza, tunacheka tunapata matumaini…nchi nzima iko hivi ni jambo jema, hatutaki miongoni mwetu aumie kwa sababu ya siasa’’ amesema Mbowe.
Amesema chama hicho kinataka wananchi waishi katika maisha ya utengamano, amani na utulivu huku akiongeza kuwa nchi ya Tanzania haiwezi kuongozwa kwa hisani ya kiongozi.
Ameongeza kuwa mafunzo waliyoyapata kwa miaka saba yakarekebishe mifumo ya utawala ili kuwa na Katiba itakayothibiti viongozi wetu na siyo viongozi watakaothibiti katiba.
‘’Tujenge taasisi imara za kuisimamia serikali kama Bunge na siyo Bunge linalosimamiwa na serikali, tuunde mahakama zitakazofanya maamuzi ya haki na kweli kwa watu wote, siyo mahakama zinazokwenda kwa maeelekezo ya kisiasa’’ amesema Mbowe.
Amefafanua kuwa watasimamia kweli na uhuru wa watu, haki za watu na demokrasia, sera kuu za CHADEMA zinajengwa katika maneno manne ambayo ni Uhuru wa watu, haki za watu, demokrasia na maendeleo ya watu.
MWISHO.
إرسال تعليق