Wanachama wa Chama kikuu cha Ushirika Mkoa wa Simiyu (SIMCU) wakifuatilia taarifa mbalimbali, wakati wa Mkutano Mkuu wa sita wa Chama hicho uliofanyika jana Mjini Bariadi. |
Wanachama wa Chama kikuu cha Ushirika Mkoa wa Simiyu (SIMCU) wakifuatilia taarifa mbalimbali, wakati wa Mkutano Mkuu wa sita wa Chama hicho uliofanyika jana Mjini Bariadi. |
Na Derick Milton, Simiyu.
Wanachama wa Chama kikuu cha Ushirika Mkoa wa
Simiyu (SIMCU) wameutaka uongozi wa Bodi ya chama hicho, kutafuta njia ya
kupunguza matumizi ya kawaida ya chama hicho na kuweka nguvu zaidi katika kuanzisha
miradi ya maendeleo.
Wakichangia taarifa mbalimbali ikiwemo taarifa ya
ukaguzi wakati wa mkutano mkuu wa sita wa Chama hicho, wanachama hao walisema
kuwa taarifa za mapato na matumizi zinaonyesha chama hicho kinaendelea kuwa na
matumizi makubwa eneo la uendeshaji.
Walisema kuwa ni wakati sasa Bodi ya Chama hicho,
kukaa kwa pamoja na watendaji kuangalia njia sahihi ya kupunguza matumizi, na
fedha nyingi kuelelekezwa katika eneo la uwekezaji na kufanya biashara.
Isaya Mwosi mmoja wa wajumbe hao kutoka Wilayani
Meatu alisema kuwa mbali na taarifa ya fedha, taarifa ya ukaguzi nayo inaonyesha
hali ya chama siyo nzuri kutokana na kupata hati isiyoridhisha.
“ Tuna wajibu kama wanachama kuwataka viongozi wa
Chama kuangalia namna ya kupunguza matumizi ya kawaida hasa eneo la kuendesha
chama, na fedha nyingi zielekezwe katika kutafuta vyanzo vipya vya mapato kwa
kuanzisha miradi mbalimbali,” alisema Mwosi.
Aidha alisema kuwa ili chama hicho kiweze
kujiendesha ni lazima kuacha kutegemea ushuru wa pamba kama chanzo kikuu cha
mapato, na badala yake kupitia viwanda vyake lazima uwekezaji ufanyike na
kianze kununua pamba kisha kuchambua.
“ Tunavyo viwanda vya Sola, Ruguru na Nassa, hivi
vyote ni mali yetu, kama chama viwanda hivi vinaweza kuwa mkombozi kwetu na
kufanyabiashara kubwa kwa kujikita zaidi katika kununua pamba na kuchambua,”
aliongeza Mwosi.
Naye Paul Lazaro alisema kuwa taarifa ya ukaguzi
wa chama hicho imetoa hati yenye mashaka, jambo ambalo aliwataka viongozi wa
Chama hicho kuangalia ni wapi pamekosewa na kufanyiwa marekebisho.
Mwenyekiti wa Chama hicho Lazaro Walwa amesema
kuwa katika kuhakikisha chama hicho kinafanya shughuli za kibiashara katika
mwaka wa fedha 2023/24 wamepanga kanzisha viwanda viwili vya kuzalisha mafuta
ya alzeti.
Mbali na hilo Walwa alisema kuwa katika mwaka huo
wa fedha chama kipo katika hatua za mwisho za kupata mkopo wa kiasi cha Sh.
Bilioni 6.4 kwa ajili ya kufufua kiwanda cha kichakata pamba cha Sola kilichopo
Wilayani Maswa.
“ Katika mipango yetu tumesema lazima kiwanda cha
sola kianze kufanya kazi na ndiyo maana leo tumekuja na ombi kwenu mtukubalie
tupate mkopo wa Bilioni 6.4 kwa ajili ya kufufua kiwanda hicho,” alisema Walwa.
Awali akitoa taarifa ya ukaguzi, Mkaguzi kutoka
shirika la ukaguzi na usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) Rodrick Kilemile
katika ukaguzi wa Chama hicho wamebaini kwepo kwa hoja zinazoathiri taarifa za
kifedha.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo, chama kinaweza
kushindwa kuendelea ikiwa pamoja na kukosa fedha za kujiendesha kutokana na
kuwa na madeni makubwa kinachodai hakuna mikakati yeyote kuweza kukusanya
madeni hayo.
“ Kutokana na hoja hizo COASCO tumetoa hadi yenye
mashaka kwa chama chenu, lakini hoja hizo zinaweza kuathiri lakini siyo kwa
kiwango kikubwa ikiwa viongozi wataweza kuzifanyia kazi,” alisema Kilemile.
Mrajisi msaidizi wa Mkoa Geofrey Mpepo akasisitiza
viongozi wa Amcos kufuata maelekezo yanayotolewa na serikali ikiwemo
kuhakikisha yanafanyika mabadiliko ya makatibu wa vyama hivyo kwa kutangaza
upya ajira na kuwapata watendaji makini.
Awali akifungua Mkutano huo, Mkuu wa Mkoa huo Dkt.
Yahya Nawanda aliwataka viongozi wa chama hicho pamoja na wale wa vyama vya
msingi vya ushirika kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi na kuwatumikia zaidi
wakulima.
MWISHO.
إرسال تعليق