Wananchi wa Mtaa wa Mwaswale, Kata ya Sima Mjini Bariadi wakiwa kando ya Gari la Jeshi la Polisi lililofika kwa ajili ya kuchukua mwili wa mwanaume aliyekutwa ameuwawa na kutupwa kwenye maji.
Mwili ukiwa ndani ya Maji katika Mtaa wa Mwaswale, Kata ya Sima Mjini Bariadi.
Na Mwandishi wetu, Bariadi.
Mapema Asubuhi ya Leo ndani ya mto ulioko kwenye msitu wa Masunzu, mtaa wa Mwaswale kata ya Sima Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Mkoani Simiyu umekutwa mwili wa mtu mmoja ambaye hakufahamika jina lake ukiwa ndani ya maji huku chanzo kikiwa hakijafahamika.
Mtu huyo ambaye ni mwanaume, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 45, amekutwa amepoteza maisha, ambapo baada ya raia wema kubaini tukio hilo wamelijulisha Jeshi la polisi lililofika na kuuchukua mwili huo kwa uchunguzi zaidi.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa, mtoto ambaye alikuwa na nguruwe, ndiye aliyegundua tukio hilo na kuanza kupiga kelele.
" Baada ya kelele za mtoto huyo, Kuna watu walikuwa kwenye ibada ya jumuiya Asubuhi kwenye nyumba Moja jirani na tukio, ndipo wakatoka na kwenda kushuhudia"
" Walipofikia kwenye tukio, kila mmoja alishangaa baada ya kukuta mwili ukiwa ndani ya Maji, wakapigwa simu kwa Mwenyekiti wa mtaa pamoja na Mtendaji wa Mtaa" anasema Juliana Sonza.
Naye Leah Ezekiel amesema tukio hilo limewasikitisha kwani hawakuwa na taarifa yoyote baada ya kijana aliyekuwa akitafuta nguruwe kukuta mwili ukielea ndani ya maji.
Amesema baada ya mwili huo kuopolewa kwenye maji, baadhi ya wananchi waliweza kuutambua mwili huo, huku akiliomba jeshi la polisi kuwachukulia hatua waliohusika na tukio hilo.
Mwenyekiti wa mtaa huo Emmanuel Paul amedhibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo amesema baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wananchi alipiga simu Polisi na kuja kuupoa mwili huo.
‘’kama mnavyoona tulifika na kuuchukua mwili kupeleka chumba cha kuhifadhia maiti, polisi wanaendelea na uchunguzi…inaonekana amenyongwa, Lakini polisi watafanya uchunguzi na watasema wenyewe...’’ amesema Mwenyekiti.
" Nimemtambua huyo mtu kwa jina la Boniphace ni mkazi wa huu mtaa, baada ya kuopolewa nimeona kama amenyongwa, lakini tunasubilia jeshi la Polisi watakuwa na Majibu baada ya uchunguzi wao" amesema Emmanuel.
Mtendaji wa mtaa wa Mwaswale, kata ya Sima Amina Yusuph Ally amesema alipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema ambapo alishirikiana Mwenyekiti wa Mtaa na polisi kata ambaye ni polisi Jamii kulijulisha Jeshi la Polisi.
Amesema tukio la mtu kuokotwa akiwa amepoteza maisha ni tukio la kwanza katika mtaa huo.
Hata hivyo mwili huo umepelekwa katika hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi, kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoani humo Blasius Chatanda alipoulizwa kuhusu tukio hilo amesema kuwa taarifa ya tukio hilo inaandaliwa na itatolewa kwa waandishi wa Habari kesho Jumatatu.
MWISHO.
إرسال تعليق