Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu ACP Blasius Chatanda, akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo Pichani) Ofisini kwake leo
Jeshi la Polisi Mkoani Simiyu limetoa taarifa ya
tukio la mwili wa mtu mmoja kukutwa ndani ya maji kwenye korongo la msimu wa
Masunzu, ambalo limetokea jana katika Mtaa wa Mwaswale kata ya Sima,
Halmashuari ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.
Mbele ya Waandishi wa habari Leo Kamanda wa Polisi
Mkoani humo, Blasius Chatanda amesema kuwa, Mwili wa mtu huyo ulitambulika kwa
jina la Boniphace Mdunguli (40-42) mkazi wa mtaa huo na alikuwa mfanyabiashara.
Kamanda Chatanda amesema kuwa baada ya kufanyika
kwa uchunguzi, imebainika kuwa marehemu aliuawa kwa kunyongwa na waya shingoni na
huku Mke wake aliyejulikana kwa jina la Salu Magambo akihusika katika mauaji
hayo.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo wa Polisi, marehemu
kabla ya kufikwa na umauti akiwa na mke wake mnamo tarehe 01/04/2023 walikuwa
pamoja kwenye mgahawa wa mke wake uliopo mtaa wa Sima na waliondoka kwa pamoja
kwenda nyumbani.
Kamanda Chatanda amesema kuwa chanzo cha tukio
hilo, ni ugomvi uliokuwepo awali kati ya marehemu na mke wake, ambapo walikuwa
wanadaina pesa ambazo marehemu alikuwa anamdai mke wake.
“ Mtuhumiwa amekamatwa na mahojiano yanaendelea
dhidi yake, lakini amekiri kuhusika na tukio hilo na alishirikiana na watu wengine
kufanya tukio hilo, tunaendelea kuwasaka hao wahusika wengine,” amesema
Chatanda.
MWISHO.
إرسال تعليق